• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Real Madrid watandikwa katika La Liga kwa mara ya kwanza msimu huu

Real Madrid watandikwa katika La Liga kwa mara ya kwanza msimu huu

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walipoteza mchuano wao wa kwanza katika kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu baada ya kucharazwa 2-1 na Espanyol ugenini mnamo Jumapili.

Raul de Tomas aliwaweka wenyeji kifua mbele katika dakika ya 17 baada ya kukamilisha krosi safi aliyoandaliwa na Adrian Embarba. Aleix Vidal aliongezea Espanyol bao la pili baada ya kumzidi Nacho maarifa na kumpiku kipa Thibaut Courtois kwa ujanja katika dakika ya 60.

Real walifutiwa machozi na mfumaji mahiri raia wa Ufaransa, Karim Benzema dakika 19 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa. Ingawa Real Madrid walipepetwa, masogora hao wa kocha Carlo Ancelotti bado wanadhibiti kilele cha jedwali la La Liga kwa alama 17 sawa na Real Sociedad na mabingwa watetezi Atletico Madrid.

Kichapo hicho kilikuwa cha pili mfululizo kwa Real kupokezwa chini ya kipindi cha wiki moja baada ya limbukeni Sheriff Tiraspol ya Moldova kuduwaza mabingwa hao mara 13 wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kichapo cha 2-1 katika mechi ya Kundi D ya kipute hicho mnamo Septemba 28, 2021 uwanjani Santiago Bernabeu.

Masogora wa Ancelotti sasa hawajashinda mechi yoyote kutokana na tatu zilizopita ikizingatiwa kwamba waliambulia sare tasa dhidi ya Villarreal katika mmchuano wao wa awali ligini.

Ingawa Benzema na Eder Militao walivurumisha makombora mazito langoni mwa Espanyol katika kipindi cha pili, fataki hizo zilidhibitiwa vilivyo na kipa Diego Lopez. Bao ambalo Benzema alifungia Real lilikuwa lake la tisa kutokana na mechi tisa za hadi kufikia sasa msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Bayern Munich wapigwa ligini kwa mara kwanza katika uwanja...

Watford wamfuta kazi kocha Xisco Munoz