• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Bayern Munich wapigwa ligini kwa mara kwanza katika uwanja wa nyumbani baada ya mechi 30

Bayern Munich wapigwa ligini kwa mara kwanza katika uwanja wa nyumbani baada ya mechi 30

Na MASHIRIKA

EINTRACHT Frankfurt walipokeza Bayern Munich kichapo cha kwanza baada ya mechi 30 za kutoshindwa kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) uwanjani Allianz Arena mnamo Jumapili kwa kuwakomoa 2-1.

Ingawa Bayern Munich waliwekwa uongozini na Leon Goretzka katika dakika ya 29, nahodha wa Frankfurt Martin Hinteregger alirejesha kikosi chake mchezoni kunako dakika ya 32 kabla ya Filip Kostic kuzamisha chombo cha wenyeji wao katika dakika ya 93.

Ushindi huo wa Frankfurt ulikuwa wao wa kwanza kusajili ligini muhula huu na wa kwanza tangu mwaka wa 2000 dhidi ya Bayern ugenini.

Licha ya kichapo, Bayern ambao walipoteza mechi katika uwanja wao wa nyumbani kwa mara ya mwisho mnamo Novemba 2019, walisalia kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa alama 16 sawa na Bayer Leverkusen na moja zaidi nyuma ya Borussia Dortmund na SC Freiburg wanaofunga orodha ya nne-bora.

Bao ambalo Goretzka aliwafungia Bayern lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na mshabuliaji matata raia wa Poland, Robert Lewandowski. Goli hilo lilikuwa la kwanza kwa Goretzka kufungia waajiri wake muhula huu.

Hinteregger alichuma nafuu kutokana na masihara ya mabeki wa Bayern na kumwacha hoi kipa Manuel Neuer katika dakika ya 32 na kusawazisha mambo.

Ingawa Bayern walipania kurejea mchezoni, juhudi zao zilizimwa na kipa wa Frankfurt, Kevin Trapp aliyepangua makombora mazito aliyoelekezewa na Lewandowski, Serge Gnabry na Leroy Sane mwanzoni mwa kipindi cha pili. Frankfurt kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama nane sawa na Stuttgart na Hoffenheim.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Njama ya Uhuru kubomoa Ruto yafichuka

Real Madrid watandikwa katika La Liga kwa mara ya kwanza...