• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Ruth kidedea akiweka rekodi mpya ya dunia mbio za 21km

Ruth kidedea akiweka rekodi mpya ya dunia mbio za 21km

Na CHRIS ADUNGO

MKENYA Ruth Chepng’etich ndiye mshikilizi mpya wa rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 21.

Hii ni baada ya mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 26 kusajili muda wa saa 1:04:02, katika mbio za Istanbul Half Marathon nchini Uturuki hapo Jumapili.

Alifanikiwa kupunguza sekunde 29 kwenye rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na Ababel Yeshaneh wa Ethiopia.

Kwa upande wa wanaume, mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 21, Kibiwott Kandie, aliweka muda bora kwenye kivumbi hicho alipokata utepe baada ya dakika 59:35.

Kandie alimpiku Mkenya mwenzake Geoffrey Kamworor, aliyeambulia nafasi ya pili katika muda wa dakika 59:38.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Kamworor – ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia katika nusu marathon – kunogesha pambano la kimataifa tangu apone jeraha alilolipata, baada ya kuhusika kwenye ajali ya pikipiki mjini Eldoret mwaka jana.

Kandie alikuwa na kundi la wanariadha watano wa kwanza kabla kuchomoka alipofika hatua ya kilomita 18.

Roncer Kipkorir wa Kenya aliridhika na nafasi ya tatu (59:46) akimzidi ujanja Walelegn Amdework wa Ethiopia katika nafasi ya nne (59:48).

Mkenya Leonard Barsoton alifunga orodha ya tano-bora kwa kusajili muda wa dakika 59:59.

Kwa upande wake, Chepng’etich alibadilishana uongozi na Yalemzerf Yehualaw wa Ethiopia mara kadhaa.

Tukio hilo lilimpa fursa ya kumsoma mpinzani wake kabla hatimaye kufyatuka zikiwa zimesalia kilomita mbili za mwisho.

“Nilikuwa na ufahamu mzuri wa eneo la mbio hizo. Sikutarajia kabisa kuvunja rekodi ya dunia kwa kupunguza sekunde 29 kwenye rekodi ya awali. Hali ya hewa ilinitatiza sana mwanzoni,” akatanguliza Chepng’etich.

“Nina furaha kubwa sana na matokeo haya ni zao la maandalizi bora ambayo nilizamia kwa muda mrefu,” akaongeza.

Yalemzerf alikuwa wa pili (1:04:40) huku Hellen Onsando Obiri akiridhika na nafasi ya tatu (1:04:51).

Brigid Kosgei – mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 42 – alikuwa wa tano (1:06:01) nyuma ya Mkenya mwingine Joan Chelimo (1:05:09).

Chepng’etich alikuwa akishiriki shindano la kwanza tangu aambulie nafasi ya pili kwenye New Delhi Marathon (1:05:06) zilizotawaliwa na Mwethiopia Yehualaw (1:04:46) mwezi Novemba.

Idadi kubwa ya wanariadha katika Istanbul Half Marathon walikuwa wamepangiwa kushiriki Ras Al Khaimah Half Marathon, kabla kufutiliwa mbali Februari sababu ya janga la corona.

Kandie alitumia mbio hizo kujipima akilenga kuwa sehemu ya kikosi cha Kenya cha 10,000m kwenye Olimpiki jijini Tokyo, Japan, baadaye mwaka huu.

“Lilikuwa shindano langu la kwanza muhula huu na nimekuwa nikijiandaa kwa miezi minne. Nilikuwa katika hali shwari; nilijua ningeshinda baada ya kumaliza kilomita tano za kwanza kirahisi,” akasema Kandie.

Aliibuka mshindi wa Valencia Half Marathon mnamo Desemba akisajili rekodi mpya ya dakika 57:32. Rekodi ya awali ya 58:01 iliwekwa na Kamworor.

Wakati huo, Kandie alimpiku Mganda Jacob Kiplimo ambaye ni bingwa wa dunia wa Nusu Marathon (57:37) na Mkenya Rhonex Kipruto aliyeambulia nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 57:49.

Chepng’etich alikuwa akishiriki shindano lake la kwanza tangu aambulie nafasi ya pili kwenye mbio za New Delhi Marathon (saa 1:05:06) zilizotawaliwa na Mwethiopia Yehualaw (1:04:46) mnamo Novemba 2020.

You can share this post!

DIMBA MASHINANI: Handiboli ya ufukweni yafaidi vijana Pwani

Mvamizi Hassan analenga magoli yasiyopungua 15 kikosini...