• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Sancho afungia Borussia Dortmund bao la kwanza katika Bundesliga msimu huu huku Bayern Munich wakipiga Mainz bila huruma

Sancho afungia Borussia Dortmund bao la kwanza katika Bundesliga msimu huu huku Bayern Munich wakipiga Mainz bila huruma

Na MASHIRIKA

FOWADI Jadon Sancho alifunga bao lake la kwanza katika kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu huu na kusaidia waajiri wake Borussia Dortmund kuchabanga VfL Wolfsburg 2-0 mnamo Jumapili.

Dortmund waliokuwa wakichezea katika uwanja wao wa nyumbani wa Signal Iduna Park, waliwekwa kifua mbele na Manuel Akanji katika dakika ya 66.

Bao la beki huyo raia wa Uswisi aliyefunga kwa kichwa, lilichangiwa na Sancho aliyecheka na nyavu mwishoni mwa kipindi cha pili aliyepokezwa krosi na Emre Can.

Ushindi wa Dortmund uliwavusha hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 25, nane nyuma ya mabingwa watetezi Bayern Munich waliopepeta Mainz 5-2 katika mechi nyingine ya Jumapili.

Mabao ya Bayern wanaonolewa na kocha Hansi Flick yalifumwa wavuni kupitia kwa Joshua Kimmich, Leroy Sane, Nikas Sule na Robert Lewandowski aliyecheka na nyavu mara mbili. Mainz walifunga magoli yao kupitia Jonathan Burkardt na Alexander Hack.

RB Leipzig na Bayer Leverkusen wanashikilia nafasi za pili na tatu jedwalini kwa alama 31 na 28 mtawalia. Kwa upande wao, Wolfsburg walishuka hadi nafasi ya sita kwa alama 24 sawa na nambari tano Union Berlin. Mechi dhidi ya Dortmund ilikuwa ya pili kwa Wolfsburg kupoteza kutokana na tatu zilizopita.

Sancho, 20, alikuwa windo la Manchester United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21. Hata hivyo, kudidimia kwa makali ya mfumaji huyo raia wa Uingereza umewafanya Man-United kumpuuza na badala yake kuanza kuyahemea maarifa ya Erling Braut Haaland wa Norway ambaye pia ni mchezaji wa Dortmund.

Kufikia sasa msimu huu wa 2020-21, Sancho anajivunia mabao sita katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

You can share this post!

Changamoto za ujauzito akiwa tineja zilimfumbua macho awe...

Atletico Madrid wacharaza Alaves 2-1 na kurejea uongozini...