• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Atletico Madrid wacharaza Alaves 2-1 na kurejea uongozini kwa jedwali la La Liga

Atletico Madrid wacharaza Alaves 2-1 na kurejea uongozini kwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

BAO la dakika za mwisho kutoka kwa fowadi wa zamani wa Barcelona, Luis Suarez, 33, liliwapa Atletico Madrid ushindi wa 2-1 dhidi ya Alaves mnamo Jumapili usiku.

Matokeo hayo yaliwarejesha masogora wa kocha Diego Simeone kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa alama 38, mbili zaidi kuliko mabingwa watetezi Real Madrid ambao wamesakata mechi mbili zaidi kuliko Atletico.

Suarez ambaye ni raia wa Uruguay, aliingia katika sajili rasmi ya Atletico mnamo Septemba 2019 na kutua kwake uwanjani Wanda Metropolitano anakozidi kushirikiana vilivyo na fowadi chipukizi Joao Felix, kulimchochea mfumaji Diego Costa kuagana na Atletico mwishoni mwa mwaka wa 2020.

Costa kwa sasa anatarajiwa kuingia kambini mwa Arsenal au Wolves mwezi huu wa Januari.

Suarez alichangia bao la kwanza la Atletico ambalo lilijazwa kimiani na Marcos Llorente katika dakika ya 41.

Alaves walisalia uwanjani na wachezaji 10 pekee katika kipindi cha pili baada ya Victor Laguardia kuonyeshwa kadi nyekundu kunako dakika ya 63.

Ingawa Felipe Augusto alijifunga na kuwapa Alaves motisha ya kurejea mchezoni katika dakika ya 84, Suarez alizamisha chombo cha wenyeji wao hao kunako dakika ya 90 baada ya kukamilisha krosi ya Felix.

Atletico walitawazwa mabingwa wa La Liga kwa mara ya mwisho mnamo 2014. Kikosi hicho kilishuka hadi nafasi ya pili kwa muda mnamo Januari 2 baada ya Real Madrid kuwapokeza Celta Vigo kichapo cha 2-0 uwanjani Santiago Bernabeu.

You can share this post!

Sancho afungia Borussia Dortmund bao la kwanza katika...

Manchester City yazamisha chombo cha Chelsea na kukaribia...