• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Scotland na Austria nguvu sawa katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia

Scotland na Austria nguvu sawa katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

GOLI la dakika za mwisho kutoka kwa John McGinn lilisaidia Scotland kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Austria mjini Hampden katika mchuano wao wa kwanza katika juhudi za kuwinda tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za 2022.

Kiungo huyo wa Aston Villa alicheka na nyavu za wageni wao katika dakika ya 85 na kuongoza Scotland kurejea mchezoni kwa kutoka nyuma mara mbili.

Grant Hanley aliwafungia Scotland bao lake la kwanza baada ya miaka minane katika dakika ya 71 na kufuta jitihada za Sasa Kalajdzic aliyefungulia Austria ukurasa wa magoli katika dakika ya 55.

Kalajdzic aliwapachikia Austria goli la pili kunako dakika ya 80 kabla ya McGinn kusawazisha mambo dakika tano kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Matokeo hayo yalikomesha rekodi duni ya Scotland ambao waliingia uwanjani wakiwa wamepoteza mechi mbili mfululizo. Sasa kikosi hicho kinajiandaa kuvaana na Israel walionyukwa 2-0 na Denmark katika mechi nyingine Mechi hiyo itachezwa Machi 28. Scotland watachuana na Faroe Islands katika mechi ya tatu ya makundi mnamo Machi 31, 2021 mjini Hampden.

Kwa upande wao, Austria wana mechi mbili za nyumbani dhidi ya Faroe Islands mnamo Machi 28 kabla ya kupimana ubabe na Denmark siku tatu baadaye.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Italia wapepeta Northern Ireland bila jasho jingi katika...

MATHEKA: Wimbi la tatu la corona lachangiwa zaidi na...