• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
STAA WA WIKI: Malkia mpya wa mbio za mita 5,000 anayefuata nyayo za Obiri

STAA WA WIKI: Malkia mpya wa mbio za mita 5,000 anayefuata nyayo za Obiri

NA GEOFFREY ANENE

BEATRICE Chebet si jina geni katika ulingo wa riadha za Kenya na hata kimataifa.

Katika miaka sita tangu Chebet ainuke, grafu yake imekuwa ya kudondosha mate.

Mzawa huyo wa Machi 5, 2000 amefanya makubwa kiasi cha kuonekana yuko mbioni kuwa malkia mpya wa mbio za mita 5,000.

Chebet alikuwa katika kikosi cha Kenya kilichoshiriki Riadha za Dunia za chipukizi walio chini ya umri wa miaka 18 jijini Nairobi mwaka 2017.

Mwaka mmoja baada ya kuambulia pakavu katika mashindano hayo, Chebet alirejea katika ulingo wa kimataifa kwa kishindo aliponyakua taji la 5000m kwenye Riadha za Dunia za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mjini Tampere, Finland mwaka 2018. Alikuwa mwanamke wa kwanza Mkenya kuvuna taji hilo na pia wa kwanza asiyetoka Ethiopia tangu 2006.

Mnamo Aprili 2019, Chebet aliongeza taji la Afrika kwa wanariadha wasiozidi umri wa miaka 20 jijini Abidjan, Ivory Coast. Hiyo ilikuwa wiki chache baada ya kutawala mbio za wanawake chipukizi (kilomita sita) kwenye Mbio za Nyika Duniani mjini Aarhus, Denmark mnamo Machi 30. Mwanzoni alikuwa amepewa shaba kwa sababu alikata utepe kwa wakati mmoja na Waethiopia Alemitu Tariku na Tsigie Gebreselama. Hata hivyo, picha ya kuthibitisha nani kati yao alivuka utepe wa kwanza ilionyesha Chebet ndiye alifanya hivyo na akazawadiwa dhahabu.

Umaarufu wa mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye hufanyia mazoezi katika eneo la Londiani kaunti ya Kericho, umeongezeka 2022. Hiyo ni baada ya kushinda medali ya fedha kwenye Riadha za Dunia mjini Eugene jimboni Oregon, Amerika mnamo Julai 23 kabla ya kutimka vizuri sana akibeba taji la michezo ya Jumuiya ya Madola mjini Brimingham, Uingereza mapema juma hili (Agosti 7).

Ukimbiaji wake umeridhisha wengi ukifanya wamwone kama mtu aliye na uwezo wa kujaza nafasi ya Mkenya mwenzake Hellen Obiri aliyevuma sana 5000m kabla ya kupanda 10000m na kisha kuingilia mbio za barabarani. Muda ndio utakuwa msema kweli iwapo atafikia kiwango cvha Obiri na hata kumpita.

  • Tags

You can share this post!

Hoki: Titans yajipatia miaka 5 ili kushiriki kipute cha...

Utaratibu wa kukagua kura wachukua muda

T L