• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Vipusa wa Ujerumani wakomoa Finland na kujikatia tiketi ya kuonana na Austria kwenye robo-fainali za Euro 2022

Vipusa wa Ujerumani wakomoa Finland na kujikatia tiketi ya kuonana na Austria kwenye robo-fainali za Euro 2022

Na MASHIRIKA

MALKIA mara nane wa Euro za wanawake, Ujerumani, walitamatisha kampeni za Kundi B katika kipute hicho kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Finland mnamo Jumamosi mjini Milton Keynes.

Vipusa hao wa kocha Martina Voss-Tecklenburg sasa wanadhibiti kilele cha Kundi B kwa pointi tisa, tatu kuliko nambari mbili Uhispania waliocharaza Denmark 1-0 ugani Brentford Community.

Finland wanaoshikilia nafasi ya 29 duniani, walitinga nusu-fainali za Euro mara ya mwisho 2005 nchini Uingereza. Waliaga makala ya mwaka huu bila alama yoyote. Uhispania iliwakomoa 4-1 kabla ya Denmark kuwatandika 1-0.

Ujerumani walisubiri hadi dakika ya 40 kufungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Sophia Kleinherne. Magoli yao mengine yalijazwa kimiani na Nicole Anyomi na Alexandra Popp ambaye amecheka na nyavu za wapinzani katika kila mojawapo ya mechi tatu zilizopita.

Sasa watashuka uwanjani Brentford kuvaana na Austria katika robo-fainali mnamo Julai 21, 2022 na watarejea Milton Keynes kwa nusu-fainali mnamo Julai 27 iwapo wataibuka washindi. Uhispania watamenyana na Uingereza katika robo-fainali nyingine mnamo Julai 20, 2022 uwanjani Amex.

Ujerumani ndio wanajivunia mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Euro za wanawake. Warembo hao wamenyanyua taji la kipute hicho mara nane huku wakitawazwa mabingwa mara sita mfululizo kati ya 1995 na 2013. Walidenguliwa kwenye robo-fainali mnamo 2017.

Walifungua kampeni zao za Kundi B kwa ushindi wa 4-0 dhidi ya wanafainali wa 2017, Denmark, kisha wakapepeta Uhispania 2-0. Ushindi dhidi ya Denmark uliwawezesha kulipiza kisasi dhidi ya kikosi kilichowabandua kwenye robo-fainali za 2017.

Mechi kati ya Ujerumani na Finland ilihudhuriwa na mashabiki 20,721, idadi hiyo ikiwa ya 13 kwa ukubwa katika historia ya Euro za wanawake.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kidero akosesha Wanga usingizi kuhusu ugavana

Wakulima wageukia maombi kukabili wizi wa zao la kahawa

T L