• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Vissel na Sagan walimwa Ayub Timbe na Ismael Dunga wakila hu Levain Cup

Vissel na Sagan walimwa Ayub Timbe na Ismael Dunga wakila hu Levain Cup

Na GEOFFREY ANENE

NDOTO ya wanasoka wa Kenya, Ayub Timbe Masika na Ismael Salim Dunga kupata matokeo mazuri katika mechi yao ya kwanza nyumbani ilizimwa baada ya Vissel Kobe na Sagan Tosu kuchabangwa Jumatano.

Kobe anayochezea Masika ilinyamzishwa 1-0 na wageni wao Tokushima Vortis ugani Noevir nayo Sagan anayosakatia Dunga ikapokea kichapo sawa na hicho kutoka kwa wageni Avispa Fukuoka kwenye Kombe la Levain.

Masika alikuwa akichezea Kobe kwa mara ya pili baada ya kuanza maisha katika sare ya 0-0 dhidi ya wenyeji Shonan Bellmare kwenye Ligi Kuu (J1 League) mnamo Aprili 17. Winga huyo aliingia katika nafasi ya kiungo Asahi Masuyama katika dakika ya 65.

Masika, 28, alipoteza angaa nafasi mbili kutokana na safu ya Tokushima kusimama imara, ingawa pia alikosa shabaha katika pasi yake ya mwisho na shuti.

Kobe walilemewa na mashambulizi ya Tokushima dakika ya 30 wakati Joel Chima Fujita aliiba pasi ya wenyeji karibu na katikati mwa uwanja na kumegea Yudai Konishi mpira kabla ya Atsushi Kawata kukamilisha shambulio hilo kupitia shuti kali.

Timu ya Kobe ilikuwa imefanyia kikosi chake kilichoanza dhidi ya Shonan mabadiliko manane. Kichapo hicho ni cha pili mfululizo cha Kobe kwenye kipute cha Levain baada ya kubwagwa 2-0 na mabingwa watetezi FC Tokyo hapo Machi 28 mjini Tokyo. Matokeo haya yanaongezea kocha Atsuhiro Miura presha. Miura hana ushindi katika michuano mitatu mfululizo katika mashindano yote. Mashabiki wamekuwa wakiitisha kufutwa kwake.

Kwa upande wake, Dunga,28, hatimaye alipata kusakata mechi yake ya kwanza nchini Japan timu yake ya Sagan ikipoteza uwanjani Ekimae Real Estate.

Kocha Kim Myung-Hwi alifanya mabadiliko mawili kwa mpigo dakika ya 66 akiwaingiza Dunga na Keita Yamashita katika nafasi za Yohei Toyoda na Chikeluba Ofoedu mbele ya mashabiki 4, 227, mtawalia.

Dunga alikaribia kuokoa waajiri wake wapya katika dakika ya 89 baada ya kipa Takumi Nagaishi kutema krosi ya Yoshiki Takahashi, lakini shuti la Mkenya huyo liligonga mlingoti. Mbelgiji Jordy Croux alikuwa amefungia Fukuoka bao dakika ya 82.

Sagan inavuta mkia kwenye Kundi A bila alama. Kashima Antlers iko kileleni kwa alama tisa ikifuatiwa na Hokkaido Consadole Sapporo (sita) na Fukuoka (tatu) katika usanjari huo.

FC Tokyo inaongoza Kundi B kwa alama tisa baada ya kulima Oita Trinita 1-0 Jumatano. Kobe, Tokushima na Oita wote wamezoa alama tatu. Wanatofautiana kwa ubora wa magoli katika usanjari huo.

Kobe itazuru Kashima Antlers nayo Sagan itakuwa ugenini dhidi ya FC Tokyo katika mechi zao zijazo ambazo ni kwenye J1 League mnamo Aprili 24.

You can share this post!

Man-City sasa wanahitaji alama nane pekee kutokana na mechi...

Refa wa kike Stephanie Frappart azidi kuweka rekodi kwenye...