• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Refa wa kike Stephanie Frappart azidi kuweka rekodi kwenye michuano ya majanadume

Refa wa kike Stephanie Frappart azidi kuweka rekodi kwenye michuano ya majanadume

Na MASHIRIKA

STEPHANIE Frappart ataongeza rekodi nyingine kwenye safari yake ya kitaaluma atakapokuwa refa wa kwanza wa kike kuwa miongoni mwa waamuzi wa soka ya wanaume ya Euro 2021.

Frappart ameteuliwa kuwa miongoni mwa maafisa wasaidizi wa mechi wakati wa kipute cha Euro kilichoahirishwa kutoka 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Refa huyo raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 37, aliweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kupuliza kipenga kwenye kipute cha wanaume cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Disemba 2020.

Mnamo Machi 2021, alikuwa pia refa wa kwanza wa kike kusimamia mechi za wanaume za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Frappart alipuliza kipenga katika fainali ya Kombe la Dunia iliyokutanisha timu ya taifa ya wanawake ya Amerika na Uholanzi mnamo 2019 kabla ya kuaminiwa fursa ya kuwa mwamuzi wa fainali ya Super Cup kati ya Liverpool na Chelsea mwaka huo.

Amewahi pia kusimamia michuano kadhaa ya wanaume katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) na kivumbi cha Europa League.

Marefa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Michael Oliver na Anthony Taylor, pia wameteuliwa kupulizwa vipenga kwenye fainali za Euro ambazo zimeratibiwa kuanza rasmi mnamo Juni 11, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Vissel na Sagan walimwa Ayub Timbe na Ismael Dunga wakila...

Man-United, Man-City na Chelsea kusambaratisha Dortmund...