• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Wanajeshi wa Ulinzi Stars wakabwa na Stima, Mathare ikipata afueni dhidi ya Nzoia

Wanajeshi wa Ulinzi Stars wakabwa na Stima, Mathare ikipata afueni dhidi ya Nzoia

Na GEOFFREY ANENE

ULINZI Stars imetupa uongozi mara mbili ikitoka sarea ya 2-2 dhidi ya Western Stima kwenye Ligi Kuu uwanjani Kericho Green, Jumatatu.

Mabingwa wa mwaka 2003, 2004, 2005 na 2010 Ulinzi waliingia mchuano na asilimia kubwa ya kuushinda. Wakiwa hawajapoteza dhidi ya Stima katika mechi 13 zilizopita (ushindi sita na sare saba), wanajeshi hao walifungua ukurasa wa mabao kupitia Oscar Wamalwa dakika ya 14.

Ulinzi, ambao kwa kawaida hutumia uwanja wa Afraha mjini Nakuru kwa mechi zao za nyumbani, walienda mapumzikoni wakifurahia uongozi huo mwembamba.

Hata hivyo, Bonaventure Muchika alipatia Stima njia ya kurejea kwenye mechi hiyo aliposababisha penalti kwa kuangusha Michael Karanor ndani ya kisanduku dakika mbili tu baada ya kipindi cha pili kuanza. Baron Oketch alichukua majukumu ya kupiga penalti hiyo na kumwaga kipa James Saruni ambaye ameitwa katika kikosi cha Harambee Stars kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2022 dhidi ya Misri na Togo mwezi ujao.

Ulinzi ilijikakamua na kurejea kifua mbele 2-1 dakika ya 75 kupitia Elvis Nandwa aliyekamilisha krosi kutoka kwa Omar Boraafya. Hata hivyo, Mbaruku Mohamed, ambaye alijaza nafasi ya James Ogada katika kikosi cha Stima dakika ya 82, alisawazisha 2-2 sekunde chache baadaye akiadhibu Ulinzi kwa kukosa kuondosha kona vizuri.

Katika mechi nyingine iliyosakatwa Jumatatu, mabingwa wa mwaka 2008 walimaliza mikosi ya kutoshinda michuano minne iliyopita kwa kuchabanga Nzoia Sugar 1-0 uwanjani Kasarani.

James Kinyanjui alipachika bao la pekee kwa kukamilisha krosi murwa kutoka kwa Tyson Otieno dakika ya 55. Ushindi huo uliendeleza rekodi nzuri ya Mathare dhidi ya Nzoia. Wanasukari wa Nzoia hawajapiga timu hiyo kutoka Nairobi tangu mwaka 2017. Nzoia nayo sasa haina ushindi katika michuano 15 zilizopita ugenini.

Baada ya mechi hizo mbili, Ulinzi imepaa nafasi moja hadi nambari nane. Ina alama 14. Imesakata mechi 10. Wanaumeme wa Stima wanapatikana katika nafasi ya 17 baada ya kurukwa na Mathare. Mathare imezoa alama nane kutokana na mechi nane nayo Stima iko alama moja nyuma baada ya kucheza mechi 11. Stima wameambulia alama mbili kutokana na michuano yao saba iliyopita.

You can share this post!

Karua ashangaa jinsi BBI itakavyosaidia kaunti kupata mgao...

Fuata utaratibu huu kuandaa keki yenye ladha tamu