• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Zidane kuagana na Real Madrid mwishoni mwa msimu

Zidane kuagana na Real Madrid mwishoni mwa msimu

Na MASHIRIKA

KOCHA Zinedine Zidane ameeleza kikosi chake cha Real Madrid kwamba ataagana nacho mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Mkufunzi huyo raia wa Ufaransa alifikia maamuzi hayo wiki moja iliyopita baada ya waajiri wake kulazimishiwa na Sevilla sare ya 2-2 ugenini katika gozi la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Hii ni mara ya pili kwa Zidane kujiuzulu kwenye wadhifa wake akiwa kocha wa Real Madrid. Aliwahi kufanya hivyo mnamo 2018 baada ya kuongoza miamba hao wa soka ya Uhispania kutia kapuni taji la tatu mfululizo kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Real wameratibiwa kupepetana na Athletic Club Bilbao kwenye La Liga mnamo Mei 16 kabla ya kukamilisha rasmi kampeni za muhula huu wa 2020-21 dhidi ya Villarreal mnamo Mei 23. Hizo ndizo zitakuwa mechi mbili za mwisho kwa Zidane kusimamia katika awamu yake ya pili ya ukocha kambini mwa Real.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, tangazo la Zidane ni zao la hofu ya kutimuliwa na Real ambao walibanduliwa na Chelsea kwenye nusu-fainali za UEFA msimu huu huku matumaini yao ya kuhifadhi ufalme wa taji la La Liga yakididimia.

Zidane alirejea ugani Santiago Bernabeu kudhibiti mikoba ya Real mwishoni mwa msimu wa 2018-19 baada ya matokeo ya kikosi hicho kushuka chini ya wakufunzi wawili – Julen Lopetegui na Santiago Solari walioaminiwa fursa za kurithi mikoba aliyoacha.

Zidane anahusishwa pakubwa na mikoba ya Juventus ambao wanatarajiwa kumpiga kalamu kocha Andrea Pirlo baada ya miamba hao wa soka ya Italia kusajili matokeo duni muhula huu. Zidane aliwahi kuwa mchezaji wa Juventus na akawa kipenzi za mashabiki wengi jijini Turin, Italia.

Zikisalia mechi mbili pekee kwa kampeni za La Liga msimu huu kukamilika rasmi, Real kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 78, mbili nyuma ya viongozi Atletico Madrid. Barcelona wanakamata nafasi ya tatu huku Sevilla wakifunga orodha ya nne-bora.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Leicester City waponda Chelsea na kutwaa Kombe la FA

JAMVI: Mbio za Ngilu kutuliza zogo, uasi katika ODM