• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Leicester City waponda Chelsea na kutwaa Kombe la FA

Leicester City waponda Chelsea na kutwaa Kombe la FA

Na MASHIRIKA

KIUNGO Youri Tielemans alifunga bao la pekee dhidi ya Chelsea na kushindia waajiri wake Leicester City ufalme wa Kombe la FA kwenye fainali iliyochezewa ugani Wembley, Uingereza na kuhudhuriwa na takriban mashabiki 21,000 mnamo Mei 15, 2021.

Nyota huyo raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 24 alivurumisha kombora kutoka hatua ya 25 katika dakika ya 63 na kumwacha hoi kipa Kepa Arrizabalaga wa Chelsea.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu 1969 kwa Leicester kunogesha fainali ya Kombe la FA. Chini ya kocha Brendan Rodgers, Leicester walimtegemea pakubwa kipa Kasper Schmeichel aliyewanyima wanasoka Ben Chilwell na Mason Mount nafasi kadhaa za wazi.

Mwishoni mwa kipindi cha pili, Wes Morgan wa Leicester alijifunga kabla ya goli hilo kubatilishwa na teknolojia ya VAR. Ushindi wa Kombe la FA unatarajiwa kumpa Rodgers motisha zaidi ya kuongoza waajiri wake kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora na hivyo kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Kocha huyo wa zamani wa Liverpool na Celtic sasa anawaandaa masogora wake kukutana tena na Chelsea katika gozi la EPL litakaloandaliwa ugani Stamford Bridge mnamo Mei 18, 2021.

Matokeo hayo yalikuwa masaibu kwa Chelsea ambao chini ya kocha Thomas Tuchel walipoteza mechi ya pili mfululizo baada ya kupigwa na Arsenal ligini mnamo Mei 12, 2021 na kujipata wakiwa na presha tele baada ya matumaini yao ya kumaliza kampeni za EPL msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora kudidimia.

Hata hivyo, Tuchel ambaye ni raia wa Ujerumani, angali na fursa nyingine ya kunyakulia Chelsea taji katika msimu wake wa kwanza ugani Stamford Bridge atakapowaongoza waajiri wake kupepetana na Manchester City kwenye fainali ya UEFA mnamo Mei 29, 2021 jijini Porto, Ureno.

Leicester walishinda Kombe la FA katika jaribio lao la tano kwenye fainali na hivyo kuwa kikosi cha 44 tofauti kuwahi kutia kapuni ubingwa wa taji hilo.

Kwa upande wao, Chelsea kwa sasa ndicho kikosi cha kwanza kuwahi kupoteza fainali ya Kombe la FA kwa misimu miwili mfululizo tangu Newcastle United wafanye hivyo mnamo 1997-98 na 1998-99.

Hii ilikuwa fainali ya 45 ya Kombe la FA kukamilika kwa matokeo ya 1-0 katika kipindi cha zaidi ya misimu 20.

Rodgers ana kuwa kocha wa kwanza baada ya Sir Alex Ferguson kuwahi kushindi Kombe la FA nchini Uingereza na Scotland.

Tielemans ndiye mchezaji wa tatu raia wa Ubelgiji kuwahi kufunga bao kwenye fainali ya Kombe la FA na kuishia kunyanyua ubingwa wa taji hilo mwaka huo, baada ya Eden Hazard mnamo 2018 na Kevin de Bruyne mnamo 2019.

Schmeichel wa Leicester ndiye kipa wa kwanza baada ya David Seaman wa Arsenal mnamo 2003 kuongoza kikosi  kushinda Kombe la FA Cup akiwa kapteni.

Mshambuliaji Olivier Giroud wa Chelsea sasa amecheza fainali ya Kombe la FA mara sita. Ni Ashley Cole (8), Ryan Giggs (7) na Roy Keane (7) ambao wamenogesha idadi kubwa zaidi ya fainali za kipute hicho.

Akiwa na umri wa miaka 37 na siku 114, beki Wes Morgan wa Leicester sasa ndiye mchezaji mkongwe zaidi wa ndani ya uwanja kuwahi kushiriki fainali ya Kombe la FA baada ya Teddy Sheringham aliyewahi kuwajibikia West Ham United mnamo 2006 akiwa na umri wa miaka 40 na siku 41.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Leeds United waponda Burnley kwenye EPL

Zidane kuagana na Real Madrid mwishoni mwa msimu