• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Azimio wacheza pata potea

Azimio wacheza pata potea

NA LEONARD ONYANGO

MUUNGANO wa Azimio unakabiliwa na kibarua kigumu kutatua mizozo kuhusu tiketi za uwaniaji huku leo Ijumaa ikiwa siku ya mwisho ya kufanya michujo.

Kulingana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), vyama vya kisiasa vinafaa kukamilisha michujo na kutatua mizozo kufikia leo.

Hali hiyo inafanya Muungano wa Azimio unaojumuisha vyama 26 kuwa katika hatari ya kushindwa kutatua mizozo tele inayohusiana na tiketi katika baadhi ya maeneo, hivyo kutoa mwanya wa kubwagwa na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Tayari Muungano wa Azimio umeandikia barua Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ukimtaka kufutilia mbali makataa ya muda wa mwisho wa kuwasilisha orodha ya wawaniaji.

Katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kaunti ya Kajiado, chama cha ODM kimesimamisha Gavana Joseph Ole Lenku huku Jubilee ikiunga mkono gavana wa zamani David ole Nkedianye. Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ametangaza kuunga mkono Bw Lenku.

Wadadisi wameonya kuwa iwapo muungano wa Azimio utasimamisha wawaniaji wawili wa ugavana Kajiado, huenda ukapoteza kiti hicho kwa mbunge wa Kajiado Kusini, Katoo ole Metito anayewania ugavana kupitia tiketi ya chama cha UDA.

Katika Kaunti ya Mombasa, vyama vya ODM na Wiper, ambavyo vyote vimo ndani ya Azimio, vimewasilisha wawaniaji wa ugavana. ODM kimempa tiketi mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir huku chama cha Wiper kikimpa gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko.

Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Simba Arati na Seneta Sam Ongeri wanawania ugavana wa Kaunti ya Kisii kupitia chama cha ODM na Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) mtawalia, ambacho pia kiko Azimio.

Muungano wa Azimio pia umesimamisha wawaniaji wawili katika Kaunti ya Nyamira ambao ni Gavana Amos Nyaribo (United Progressive Alliance) na mwekahazina wa ODM, Timothy Bosire (ODM). Hatua ya Azimio kusimamisha wawaniaji wawili huenda ikatoa mwanya kwa Bw Walter Nyambati wa UDA kushinda kiti hicho.

Vigogo wa Azimio pia hawajafikia mwafaka kuhusu ni nani kati ya naibu gavana wa zamani wa Nairobi Polycarp Igathe (Jubilee) na Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi atamenyana na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja wa UDA katika kinyang’anyiro cha ugavana.

Kinara wa ODM Raila Odinga ameshikilia kuwa umaarufu wa Bw Wanyonyi uko juu ikilinganishwa na Bw Igathe. Lakini chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta kinasisitiza kuwa hakitaachia ODM urais na ugavana wa Nairobi.

Mvutano baina ya ODM na Jubilee kuhusu viti vya ubunge katika baadhi ya maeneobunge jijini Nairobi pia ungali haujatatuliwa.

Kulingana na mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi George Aladwa, mvutano baina ya washirika hao wakuu wa Azimio ndio umesababisha chama hicho kuahirisha kura za mchujo. Mchujo wa ODM jijini Nairobi unatarajiwa kufanyika leo.

Jana Alhamisi, Rais Kenyatta aliongoza Baraza Kuu la Azimio ambapo waliafikiana kuunda kamati itakayoshughulikia malalamishi kuhusu uchaguzi ndani ya muungano huo. Baraza hilo liliidhinisha kuundwa kwa kamati maalumu itakayoanzisha mchakato wa kusaka mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

Katika mkutano huo, Baraza Kuu liliagiza Kamati Kuu ya Kitaifa inayoongozwa na Bw Oparanya, kuandaa mikakati kuhusu namna muungano huo utaendesha kampeni zake kuanzia Mei 29, mwaka huu. Shughuli za kamati hiyo huenda zikakinzana na majukumu ya sekretariati iliyobuniwa na Bw Odinga kuendeleza kampeni zake.

Sekretariati ya kampeni za Bw Odinga inaongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju.

Viongozi wanaomezea mate nafasi ya mwaniaji mwenza wa Bw Odinga ni Bi Karua, mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth, Gavana wa Machakos Alfred Mutua na Bw Musyoka.

  • Tags

You can share this post!

Wauzaji mitumba waiomba serikali ipunguze ushuru

Aubameyang abeba Barcelona dhidi ya Real Sociedad ligini

T L