• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Bunge kujadili BBI kwenye kikao maalum

Bunge kujadili BBI kwenye kikao maalum

Na SAMWEL OWINO

BUNGE la Taifa linatazamiwa kuwa na kikao maalum kwa siku tatu kujadili ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) kutoka kwa kamati ya kisheria iliyojumuisha Bunge na Seneti.

Vikao hivyo maalum vitaandaliwa Aprili 27 na 28 kabla ya vikao kurejelewa rasmi mnamo Mei 4.

Kiongozi wa wengi John Mbadi alithibitishia Taifa Leo kwamba wamekubaliana kuwa na vikao hivyo maalum ambavyo pia vinatazamiwa kujadili Mswada kuhusu Ugavi wa Mapato uliofanyiwa marekebisho na Seneti Jumanne.

“Naam, tutakuwa na kikao maalum tarehe 27 kujadili Mswada kuhusu Ugavi wa Mapato, kisha tarehe 28 na 29 tutajadili BBI,” Bw Mbadi alieleza Taifa Leo.

Spika wa Bunge la Taifa Justin Muturi, hata hivyo, alisema hakuna kikao maalum ambacho kimepangwa na bunge.

Wiki iliyopita, Bw Muturi alisema kuwa hajapokea ombi lolote kuhusu kikao maalum kutoka kwa kiongozi yeyote kuhusiana na ripoti ya BBI.

“Sijapokea ombi lolote kama hilo, lakini likija, nitakabiliana nalo ipasavyo,” alisema Spika Muturi.

Kiongozi wa wengi Amos Kimunya hakujibu simu wala jumbe zetu kuhusiana na kikao hicho maalum.

Haya yamejiri wakati kamati inayoshughulikia Mswada wa BBI inatazamiwa kwenda likizo hii leo katika Hoteli ya Windsor ili kuandaa ripoti ya mwisho kuhusu BBI.

Likizo hiyo imewadia huku kukiwa na ripoti kwamba kamati hiyo imegawanyika kuhusu ama kuirekebisha ripoti hiyo iliyopitishwa na mabunge 43 ya kaunti au kuiwasilisha jinsi ilivyo bungeni.

Taifa Leo imethibitisha kwamba wataalam wawili wa kisheria walioteuliwa na kamati hiyo kutoa ushauri kuhusu vipengele vikuu, watakutana na wanachama kabla ya kamati hiyo kuandaa ripoti ya mwisho itakayowasilishwa ili kujadiliwa.

Kamati hiyo iliwateua Profesa Patricia Kameri-Mbote na Dkt Collins Odote kama wataalam wa kuishauri kuhusu masuala kama vile aina ya Mswada huo, ushirikishwaji wa umma na upeo wake, namna ya kuidhinisha Mswada huo, suala kuu kuhusu Mswada, maswala ya kura ya maoni pamoja na hali ya malalamishi kortini kuhusu Mswada huo.

Ajenda kuu kuhusu mswada huo ni mazungumzo kutoka kwa wataalam kuhusu masuala sita muhimu, kisha wanachama wa kamati watajadili matokeo ya ripoti hiyo kabla ya katibu na wataalam kuandaa ripoti ya mwisho.

Duru zinaashiria kuwa wataalam wameonya dhidi ya kufungua tena nakala hiyo na pia wametoa uamuzi mkali dhidi ya maeneobunge 70 wakisema suala hilo linapaswa kushughulikiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Swali kuhusu iwapo ripoti hiyo inastahili kufanyiwa marekebisho au la pamoja na maeneobunge 70 ya ziada, yamekuwa masuala tata katika ulingo wa kisiasa huku wabunge wanaoegemea ODM wakihisi kwamba hawakufanyiwa haki katika ugavi wa maeneobunge.

Kulingana na duru, kamati hiyo inakabiliwa na utata kuhusu iwapo maoni ya wataalam yanapaswa kutumiwa katika mchakato huu wa kurekebisha katiba au yanapaswa tu kuwa sehemu ya rekodi za bunge ambazo zinaweza kutumiwa katika marekebisho ya kikatiba katika siku za usoni.

You can share this post!

RAILA AMTATIZA UHURU AKILI

Watu 30 pekee wahudhuria mazishi ya mume wa Malkia