• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
CECIL ODONGO: Raila asikate tamaa kuuza sera zake Mlima Kenya

CECIL ODONGO: Raila asikate tamaa kuuza sera zake Mlima Kenya

Na CECIL ODONGO

Kinara wa ODM Raila Odinga hafai kukata tamaa katika jitihada zake za kupata uungwaji mkono kutoka eneo la Mlima Kenya licha ya dhana ya miaka nenda miaka rudi kwamba hauziki kisiasa miongoni mwa jamii za GEMA.?

Wiki jana, kampeni za Bw Odinga zilivurugwa katika eneo la Githurai na vijana wenye hamaki huku kukiwa na madai kwamba baadhi ya wanasiasa wa Tangatanga walihusika kufadhili vurugu hizo.

Kiongozi huyo alikuwa akivumisha ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) baada ya kukutana na wazee katika Kaunti ya Kiambu.

Kwanza, Kenya ni nchi ya kidemokrasia ambako mwanasiasa yupo huru kuzuru eneo lolote kujitafutia uungwaji mkono. ? Kwa hivyo, matamshi ya baadhi ya wabunge kutoka uliokuwa mkoa wa Kati kwamba wapigakura wamekataa Bw Odinga hayana mashiko na yanalenga kuwachochea wapigakura dhidi yake.

Japo kwa kiasi fulani eneo hilo sasa linamwaabudu Naibu Rais Dkt William Ruto kisiasa hiyo si sababu tosha ya kuzuia safari zake au kuvuruga mikutano yake kwa kutumia makundi ya vijana wa Tangatanga.

Aidha ni kweli kwamba kwenye chaguzi za 1997, 2007, 2013 na 2017, kigogo huyo wa siasa za upinzani amekuwa akipata kura chache mno eneo la Kati. ? Hiyo ni kwa sababu wanasiasa wanaowania viti mbalimbali wamekuwa wakijizolea uungwaji mkono kwa kwa kumtusi Bw Odinga na kumshabikia Rais Uhuru Kenyatta na mtangulizi wake Mwai Kibaki.

Kuna wabunge kutoka kaunti za Mlima Kenya ambao wamehudumu mihula miwili na zaidi lakini hakuna maendeleo yoyote ya maana waliyofanyia raia. Kiini kuchaguliwa kwao kila mwaka wa kura ni kutokana na matusi na kejeli dhidi ya Bw Odinga na pia kumsawiri kama adui mkubwa wa eneo hilo.

Hata hivyo, kuelekea uchaguzi kuu ujao, wamegundua mambo ni tofauti kutokana na ukuruba wa kisiasa kupitia ‘handisheki’ uliopo kati ya Rais Kenyatta na kiongozi huyo wa chama cha ODM.

Hiyo ndiyo maana wengi wao sasa wamekimbilia upande wa Naibu Rais Dkt William Ruto sio eti kwa sababu ya rekodi yake ya maendeleo bali kupata fursa ya kuendeleza siasa za matusi dhidi ya Bw Odinga kama njia ya kujipendekeza kwa raia.

Iwapo kwa kweli wanadai Dkt Ruto ameendeleza eneo hilo na anafaa kuchaguliwa 2022 kwa nini nyaraka ambazo wamekuwa wakiandikia Rais Kenyatta zinasisitizia kuporomoka kwa kilimo cha kahawa, majani chai, miraa na uchumi nzima wa eneo la Kati?

Ni kinaya kudai kwamba Rais ameporomosha uchumi wa eneo hilo na wakati huo huo kusisitiza Dkt Ruto ni mchapakazi ilhali wawili hao walihudumu katika utawala moja kwa miaka tisa sasa.

Kulingana na takwimu za upigaji kura za 2007, 2013 na 2017 ambapo alipata zaidi ya kura milioni sita, Bw Odinga akipata tu asilimia 30 pekee za eneo la Kati na kudumisha ngome zake za kisiasa basi hakuna mwaniaji wa Urais atakayembwaga.

Huenda kambi ya Tangatanga wamegundua hilo linawezekana kutokana na ushirikiano kati ya Rais na Bw Odinga ikizingatiwa eneo hilo huenda lisitoe mwaniaji wa Urais 2022.

Hata Dkt Ruto alikuwa anachukiwa sana na wapigakura wa GEMA baada ya 2007, lakini wakamkumbatia 2013 alipoanza kushirikiana na Rais Kenyatta.

Jambo la muhimu ambalo wapiga kura wa Mlima Kenya wanafaa wajifunze ni kujihadhari na wanasiasa wanaomimina matusi dhidi ya Bw Odinga ili wachaguliwe ilhali hawatimizii wananchi miradi ya maendele.

Pia vijana wa eneo hilo na kote nchini wanafaa wajihadhari na wanasiasa wanaowalipa pesa kidogo ili wazue ghasia mikutanoni.? Bw Odinga aruhusiwe kujiuza eneo la Kati na hata wawaniaji wengine kama Dkt Ruto pia wawe huru kusaka kura katika ngome yake ya Nyanza.

You can share this post!

MARY WANGARI: Uwekezaji zaidi kisayansi na kiteknolojia...

Sonko atupwa ndani siku tatu