• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Facebook yaadhibu wafuasi wa Museveni

Facebook yaadhibu wafuasi wa Museveni

Na DAILY MONITOR

KAMPALA, Uganda

WATU zaidi ya 50 ambao wamekuwa wakimpigia debe Rais Yoweri Museveni mitandaoni wamezuiliwa kutumia mtandao wa Facebook, siku tatu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Alhamisi, wiki hii.

Wafuasi wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), wikendi walidai kuwa akaunti zao za Facebook walizokuwa wakitumia kuwashambuliwa wapinzani wa Rais Museveni zilifungwa katika hali ya kutatanisha.

“Ni aibu kwa mataifa ya Magharibi ambayo yanadhani kwamba yanaweza kuwalazimishia Waganda kiongozi ambaye ni kikaragosi chao. Hata wakifunga akaunti za Facebook za wanaharakati wa chama cha NRM, Rais Kaguta Museveni bado atashinda uchaguzi mkuu ujao,” Don Wanyama, mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha rais, aliambia wanahabari wikendi.

Wanyama alidai kuwa mataifa ya kigeni yanafadhili wawaniaji wa upinzani kwa lengo la kutaka kumng’oa Rais Museveni kutoka mamlakani.

Wafuasi wa Museveni walidai kuwa kampuni ya Facebook iliondoa akaunti zao kufuatia ombi la mwaniaji wa urais kupitia chama cha National Unity Platform (NUP) Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.

“Facebook walifunga akaunti zetu baada ya Bobi Wine kuwaomba kufanya hivyo,” akadai mmoja wa wanablogu wa chama cha NRM.

Wanaharakati hao wa NRM sasa wanataka Rais Museveni kupiga marufuku matumizi ya Facebook nchini Uganda wakati wa uchaguzi.

Lakini katibu mkuu wa NUP Lewis Rubongoya alikanusha madai kuwa Bobi Wine alishirikiana na Facebook kufunga akaunti za wanaharakati wa NRM.

“Tumekuwa na shughuli nyingi hivi karibuni na hatuna wakati wa kujihusisha na siasa chafu,” akasema.

Waganda sasa wameelezea wasiwasi wao kuwa huenda wakazimiwa intaneti wakati wa uchaguzi.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2016, serikali pia ilizima inteneti kutokana na madai ya kujaribu kuzuia usambazaji wa taarifa ambazo huenda zingesababisha kuzuka kwa fujo.

Miongoni mwa watu ambao akaunti zao za Facebook zimezimwa ni ile ya mshauri wa rais Jennifer Nakangubi, maarufu Full Figure.

Baada ya kuzuiliwa kukutana na watu ili kuepuka kusambaza virusi vya corona, Bobi Wine amekuwa akiendesha kampeni zake kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Instagram.

Lakini mara kadhaa chama cha NUP kimekuwa kikilalamikia chama tawala cha NRM kwa kujaribu kudungua akaunti zake.

Iwapo atachaguliwa, Museveni, 76, atapata fursa ya kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa muhula wa sita.

Mbali na Bobi Wine, Rais Museveni anamenyana na wawaniaji wengine 10, akiwemo mwanamke mmoja.

Kwa kawaida Facebook huondoa akaunti mtumiaji anapochapisha mambo yanayosababisha uhasama au vurugu haswa wakati wa uchaguzi.

Facebook, wiki iliyopita, ilifunga akaunti ya kiongozi wa Amerika anayeondoka Donald Trump kwa kuchapisha kauli zilizochochea wafuasi wake kuvamia jengo la Bunge la Capitol.

Kampuni ya Facebook haijatoa taarifa kuhusu sababu yake ya kufunga akaunti za wafuasi wa NRM.

You can share this post!

Ruto ashauriwa kuungana na Kalonzo kupenya Ukambani

Chadema washindwa kumshtaki Magufuli ICC