• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Gavana atoa onyo haitakuwa rahisi kumuondoa 2022

Gavana atoa onyo haitakuwa rahisi kumuondoa 2022

Na Wycliffe Nyaberi

GAVANA wa Nyamira Amos Nyaribo ameonya wanasiasa wanaomezea mate wadhifa wake, kwamba haitakuwa rahisi kumngoa mamlakani licha ya upole wake anapozungumza hadharani.

Bw Nyaribo amesisitiza sifa hiyo haipaswi kutumiwa na wapinzani kumsaili kama kiongozi asiyefaa kuwatumikia wenyeji wake, kwani anazidi kujizatiti kila uchao kuboresha maisha ya wakazi.

Siasa za ni nani bora kukitwaa kiti cha ugavana Nyamira kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, zilishamiri pakubwa mazishi ya Bi Jane Munda, mkewe mwekahazina wa kitaifa wa chama cha ODM, Bw Timothy Bosire.

Hafla hiyo ya juzi kijijini Nyamwanga, ilitoa jukwaa kwa wanaolenga kumbandua Gavana Nyaribo kujigamba mbele ya kinara wa ODM Raila Odinga na viongozi wengine waliohudhuria.

Mbunge wa Borabu Ben Momanyi na aliyekuwa mbunge wa zamani wa Kitutu Masaba Walter Nyambati walitumia fursa hiyo kumtahadharisha Bw Nyaribo kuwa kiti chake kimo hatarani kunyakuliwa.

Walimweleza peupe kuwa watamenyana naye debeni. “Nyaribo wewe sasa kazi yako imekwisha. Si unaskia wengine wanakuja. Tutapambana na wao hapo nje,” akasema Bw Nyambati.

Naye mbunge wa Borabu Ben Momanyi, ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Bw Nyaribo siku nenda siku rudi tangu arithi kiti kilichoachwa wazi na marehemu John Nyagarama, hakuachwa nyuma kuelezea azma yake.

“Hivi karibuni tutakuwa wapinzani. Nilisikia mama mmoja akimwambia Bw Bosire kuhusu ndoto ya kumwombea awe gavana. Ni kama mama huyo hakumaliza kuota na ambacho hakumweleza ni kuwa ikiwa si yeye, basi gavana wa Nyamira atakuwa Bw Ben Momanyi,” mbunge huyo akazungumza kurejelea waliokuwa wakimpigia upatu mwekahazina huyo wa ODM kuwania ugavana.

Licha ya kufiwa na mkewe, Bw Bosire vilevile alionyesha nia ya kuendelea kuwatumikia Wakenya baada ya kukipoteza kiti cha ubunge katika uchaguzi wa 2017.

“Marehemu mke wangu alisimama nami kila wakati katika siasa na alikuwa wa maana zaidi hata nilipopoteza kiti cha ubunge wa Kitutu Masaba. Nitazidi kuazimia kuwatumikia tena Wakenya kitaifa na ngazi ya kaunti katika wadhifa wowote watakaonipa,” akasema Bw Bosire kwenye ujumbe wa kumuaga mpenzi wake.

You can share this post!

Msaka kazi ashtakiwa kuwapora wanabenki watatu Sh255,000...

Kamishna atishia kufunga baa zinazokiuka kanuni za kuzuia...