• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
JAMVI: Huenda miswada isaidie Uhuru, Raila kuandaa refarenda

JAMVI: Huenda miswada isaidie Uhuru, Raila kuandaa refarenda

Na DAVID MWERE

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaweza kutimiza lengo lao la nchi kuandaa kura ya maamuzi hata kama Mahakama ya Rufaa itakataa kuidhinisha ifanyike.

Hii ni kwa sababu Miswada kadhaa ya kubadilisha katiba ya Kenya iliyo na mapendekezo sawa inaendelea kupitia mchakato wa bunge na baadhi yake inapangwa kujadiliwa bunge likirejelea vikao mwezi ujao baada ya likizo ndefu.

Ingawa haina maelezo mengi kama Mswada wa Mpango wa Maridhiano BBI wa 2020, ambao unalenga kubadilisha ibara 70 za katiba ya 2010, Miswada hiyo iliyoandaliwa na wanasiasa kutoka mirengo yote ya kisiasa, inaweza kushughulikia baadhi ya mapendekezo ya BBI.

Miswada hiyo iliundwa kati ya 2017 na 2019, hata kabla ya Mswada wa BBI uliozinduliwa Kisii Oktoba 21, 2020.

Sawa na BBI, Miswada hiyo, iwapo itaidhinishwa na bunge, itahitaji kura ya maamuzi kabla ya kuwa sheria.Baadhi ya yanayopendekezwa kwenye Miswada hiyo ni mawaziri kuwa wabunge na haja ya kutatua hitaji la usawa wa jinsia.

Mingine ni kufanya Hazina ya Maeneo Bunge kuwa hitaji la kikatiba na kufanyia mabadiliko mfumo wa uchaguzi.Pendekezo la mbunge maalum, David Sankok, kufuta hitaji la thuluthi mbili ya wawakilishi kutokuwa wa jinsia moja lilikataliwa na kamati ya bunge kuhusu haki na sheria.

Mnamo Septemba 19, 2019, kamati iliyosimamiwa na mbunge wa Baringo Kaskazini, Bw William Cheptumo ilipendekezea bunge mswada wa Bw Sankok usichapishwe.

Hata hivyo, mwenyekiti mwenza wa ofisi ya BBI, Bw Junet Mohamed, alikataa kusema iwapo Miswada hiyo mitatu itachukua malengo ya BBI kwa kuwa hakujibu maswali yetu.

Lakini kiongozi wa wachache katika bunge la taifa, Bw John Mbadi ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM, alisema ana matumaini Mahakama ya Rufaa itafungulia BBI njia huku akisema kwamba chama chake hakikushauriwa kuhusu Miswada iliyo mbele ya bunge.

“Akili yangu iko kwa BBI na matumaini yangu ni kwamba Mahakama ya Rufaa itabatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu,” alisema Bw Mbadi.

Waandalizi wa BBI walikata rufaa baada ya majaji watano wa Mahakama Kuu kuzima mchakato wa kubadilisha katiba wa BBI wakisema haukuwa wa kikatiba.

“Kama mambo hayataenda tulivyopanga, kama chama, tutashauriana na kukubaliana mwelekeo ambao tutachukua. Lakini inafaa kueleweka kwamba Miswada iliyo mbele ya bunge iliandaliwa bila viongozi wa vyama kushauriwa. Kwa hivyo, hatuwezi kudandia Miswada ya watu,” alisema.

Mbunge wa Tiaty, Bw Kassait Kamket alikuwa amependekeza marekebisho ya Katiba kubuni wadhifa wa Waziri Mkuu na mawaziri kuteuliwa miongoni mwa wabunge inavyopendekezwa katika BBBI.

Kwenye mswada wake, Bw Kamket pia alipendekeza wadhifa wa kiongozi wa upinzani urejeshwe katika Bunge la Taifa. Tofauti ya Mswada wake na BBI, ni kutaka tarehe ya uchaguzi mkuu iahirishwe hadi Jumanne ya pili ya Desemba kila baada ya miaka mitano.

Kwa wakati huu, katiba inasema uchaguzi mkuu unafaa kufanyika Jumanne ya pili ya Agosti kila baada ya miaka mitano.

You can share this post!

Brazil na Ivory Coast kuumiza nyasi leo

Masaibu yalivyomwandama Jaji Muchelule kwa miaka 14