• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Brazil na Ivory Coast kuumiza nyasi leo

Brazil na Ivory Coast kuumiza nyasi leo

YOKOHAMA, Japan

BAADA ya kushinda mechi zao za ufunguzi katika Kundi D kwenye Olimpiki zinazoendelea nchini Japan, Brazil na Ivory Coast watashuka leo dimbani kuumiza nyasi za uwanja wa Yokohama.

Brazil ambao ni mabingwa watetezi, watakuwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 4-2 dhidi ya Ujerumani mnamo Alhamisi iliyopita.

Kwa upande wao, Ivory Coast watajibwaga ulingoni wakiwa na motisha ya kupepeta Saudi Arabia 2-1 katika gozi la awali.

Ivory Coast walijikatia tiketi ya kunogesha Olimpiki licha ya Misri kuwapokeza kichapo cha 2-1 kwenye fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 23 mnamo 2019.

Chini ya kocha Andre Jardine ambaye amewahi kudhibiti mikoba ya Sao Paulo, Brazil watategemea zaidi maarifa ya wavamizi Richarlson Andrade na Paulinho Bezerra waliowafungia mabao dhidi ya Ujerumani.

Ni mara moja pekee tangu 1976 ambapo kikosi cha Brazil kimeshindwa kutia kapuni medali ya aina yoyote kwenye Olimpiki.

Jardine ameongoza Brazil kushinda mechi tatu zilizopita ambazo zimeshuhudia miamba hao wakijizolea jumla ya mabao 12 na nyavu zao kutikiswa mara nne pekee.

Kwingineko, mabingwa wa 2012 Ufaransa watamenyana na Afrika Kusini mjini Saitana katika mechi ya Kundi A ambayo wana ulazima wa kushinda ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele.

Huku Ufaransa wakilenga kujinyanyua baada ya kupigwa 4-1 na Mexico mnamo Alhamisi, Afrika Kusini watakuwa wakipania kujitoa topeni baada ya kucharazwa 1-0 na wenyeji Japan katika mechi iliyopita.

Chini ya kocha Sylvain Ripoll, Ufaransa ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu wa kutwaa dhahabu ya Olimpiki mwaka huu baada ya kushindwa kutinga fainali ya Euro 2019 na 2021 kwa chipukizi wa Under-21.

Dhahabu ya pekee ambayo Ufaransa wanajivunia kwenye Olimpiki ni ile waliyojizolea mnamo 1984. Tangu wakati huo, wamewahi kufuzu kwa fainali ya michezo hiyo mara moja pekee – 1996.

Ilivyo, Ufaransa wako pazuri zaidi kushinda mchuano wa leo ikizingatiwa kwamba maandalizi ya Afrika Kusini wanaotiwa makali na kocha David Notoane yametatizwa pakubwa na visa vya maambukizi ya virusi vya corona kambini mwao.

Katika Kundi C, Argentina watachuana na Misri mjini Sapporo Dome. Huku Misri wakijivunia kusajili sare tasa dhidi ya Uhispania katika mechi iliyopita, Argentina waliotawazwa mabingwa mnamo 2004 na 2008, watajitosa uwanjani wakilenga kujinyanyua baada ya kulazwa 2-0 na Australia mnamo Alhamisi.

RATIBA YA SOKA YA WANAUME (Leo):

KUNDI A: Ufaransa vs Afrika KusiniJapan vs MexicoKUNDI B: New Zealand vs HondurasRomania vs Korea KusiniKUNDI C: Misri vs Argentina Australia vs UhispaniaKUNDI D: Brazil vs Ivory CoastSaudi Arabia vs Ujerumani

You can share this post!

Waganga waonywa dhidi ya kutibu wasichokielewa

JAMVI: Huenda miswada isaidie Uhuru, Raila kuandaa refarenda