• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Joho amruka Kingi kuhusu kugura ODM

Joho amruka Kingi kuhusu kugura ODM

Na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho ametofautiana na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi kuhusiana na kuendelea kutegemea Chama cha ODM kwa siasa za Pwani.

Huku Bw Kingi akionekana kushinikiza Pwani kujisimamia na kutokuwa ndani ya ODM moja kwa moja, Bw Joho jana alitangaza kuwa yeye atashikilia chama hicho kinachoongozwa na Bw Raila Odinga hadi mwisho.

Bw Joho aliongeza kuwa azma yake ya kuwa Rais wa nchi hii pia itakamilika kupitia chama hicho hicho cha ODM ambacho alisema atakitumia kuwania urais mwaka wa 2022.

“Nilikuwa mbunge wa eneo la Kisauni na nikawa Gavana wa kwanza wa Mombasa kwa mihula miwili kupitia chama cha ODM. Nimeunga chama cha ODM miaka mingi sana. Na leo natuma ujumbe wajue kuwa niko katika kinyang’anyiro cha kupigania Urais kupitia chama cha ODM,” akasema Bw Joho jana Alhamisi alipokuwa anazungumza katika Uwanja wa Mbuzi eneo la Kongowea, Nyali.

Aidha, magavana hao wawili pia wametofautiana katika azma yao ya kuwania urais kwani katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Kingi alisema kuwa yeye atawania urais lakini hatotumia ODM.

Bw Kingi alisema kuwa kwa muda sasa Pwani imekosa uwakilishi wa kisawasawa katika meza ya kitaifa kwa sababu ya kuwakilishwa kupitia vyama vyingine kikiwemo ODM.

“Mimi sitowakilisha matakwa yangu ya kuwania kiti hicho kupitia ODM. Hilo liwe wazi kabisa. Azma ya kuwania kiti hicho bado ipo lakini haitotimia kupitia ODM. Kwa sasa mwelekeo wangu ni kuhakikisha kuwa tunapata chama chetu cha Pwani,” akasema Bw Kingi awali.

Alhamisi, Bw Joho alisema kuwa njia atakayotumia ni kuhakikisha kuwa anaungwa mkono na viongozi wengine wa ODM akiwemo Bw Odinga.

“Wale ambao tumewaunga tunawaambia kuwa ni wakati wao kutuunga sisi sasa. Tumewaunga mkono kwa muda sana,” akasema Bw Joho.

Azma ya Bw Joho hata hivyo itakuwa ngumu kwani Gavana wa Kakamega Wycliff Oparanya naye pia ametangaza kuwa anataka tiketi hiyo ya kuwania Urais.

Wawili hao wanatarajiwa kupambana na Bw Odinga ambaye ndiye kinara wa chama na mshindani mkuu wa Naibu Rais William Ruto.

Kufikia sasa, kinyang’anyiro hicho cha kutaka urais kimeonekana kuelekea kuwa kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga. Wengine ambao wanataka kiti hicho ni pamoja na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka pamoja na kinara wa chama cha KANU Gideon Moi.

  • Tags

You can share this post!

Murathe sasa akiri kauli ya Kang’ata ni kweli kuhusu BBI...

Wataalam waanza kusaka kiini cha corona jijini Wuhan