• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Jubilee ni kisiki katika utekelezaji katiba – Maraga

Jubilee ni kisiki katika utekelezaji katiba – Maraga

Na VALENTINE OBARA

JAJI Mkuu David Maraga, amelaumu Serikali ya Jubilee kwa kuhujumu juhudi za utekelezaji wa katiba iliyopitishwa mwaka wa 2010.

Huku shinikizo ikizidi kutoka kwa baadhi ya viongozi, mashirika ya kijamii na wananchi wanaotaka katiba hiyo ifanyiwe marekebisho, Jaji Maraga anasema tatizo kuu zaidi kwenye katiba halihusu yaliyomo bali watu wanaopewa mamlaka makubwa katika utekelezaji.

Akihutubu Jumanne kwenye mkutano wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, Bw Maraga alisema vitengo vitatu vya serikali ambavyo ni Afisi ya Rais, Bunge na Mahakama vina majukumu muhimu katika kutekeleza katiba.

Hata hivyo, alieleza kuwa jukumu kubwa zaidi limo mikononi mwa Afisi ya Rais ambayo hutegemewa kubuni marekebisho ya sheria zinazowezesha utekelezaji wa katiba mpya ipasavyo, na pia kutoa mchango kwa njia nyinginezo katika utekelezaji huo.

“Vitengo vya Bunge na Afisi ya Rais visipodhibitiwa, huwa vinashawishiwa na wanasiasa pamoja na watu wengine wenye ushawishi mkuu katika siasa za nchi ili kutekeleza katiba kiholela kwa kutimiza tu sehemu rahisi zisizokuwa na utata, huku vikiwa na lengo la kulinda masilahi yao ya kibinafsi. Hivi ndivyo wamefanya Kenya,” akasema.

Utekelezaji wa katiba ulianza kushika kasi katika mwaka wa 2013 wakati Serikali za Kaunti zilipoanza kushika usukani, huku pia sheria nyingi zilizolenga kufanikisha utekelezaji huo zikianza kupitishwa wakati huo.

Ni katika mwaka huo ambapo Jubilee iliingia serikalini ikiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto ambao walitangazwa tena washindi wa urais kwenye uchaguzi wa 2017.

Kulingana na Bw Maraga, mifano ya sehemu za katiba ambazo Jubilee imeshindwa au kukataa kufanikisha ni zile zinazolenga kufanikisha usawa wa kijinsia katika uongozi, kuangamiza ufisadi na ukwepaji sheria, na kuwezesha uchaguzi kufanywa kwa njia ya haki na uaminifu.

“Licha ya kuwa Kielelezo cha Tano cha Katiba kiko wazi kuhusu sheria za utekelezaji wa sehemu mbalimbali za katiba zilistahili kupitishwa katika kipindi cha miaka mitano, sasa karibu miaka kumi imepita ilhali sheria kuhusu usawa wa jinsia uongozini haijapitishwa. Kwa nini? Kwa sababu ni wazi sheria aina hiyo itaathiri na kutatiza masilahi ya Wakenya wenye ushawishi mkubwa katika siasa za kitaifa,” akasema.

Rais huyo wa Idara ya Mahakama nchini alisema iwapo mwenendo huu utazidi kushuhudiwa, taifa litaendelea kupitisha katiba bila utekelezaji wake.

Wito wa kurekebisha katiba umekuwa ukipigiwa debe na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga ingawa umepingwa vikali na Dkt Ruto pamoja na wandani wake wanaodai ni njama za kuvuruga mipango ya Naibu Rais kumrithi Rais Kenyatta mamlakani ifikapo mwaka wa 2022.

Rais Kenyatta amekuwa akionyesha dalili za kuunga mkono misimamo ya Bw Odinga tangu walipoweka mwafaka wa maelewano.

You can share this post!

Raila amtembelea Gavana Laboso hospitalini London

Wazazi wamshangaa msichana aliyekunywa sumu shuleni

adminleo