• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 12:42 PM
Kambi ya Ruto yainua mikono

Kambi ya Ruto yainua mikono

Na ONYANGO K’ONYANGO
 
WASHIRIKA wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto ambao wamekuwa wakipinga kura ya maamuzi kuandaliwa kabla ya uchaguzi Mkuu wa 2022, sasa wamekubali ifanyike kabla ya uchaguzi huo.
Viongozi hao walibadilisha msimamo wao siku moja tu baada ya kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, kusisitiza kuwa ni lazima kura ya maamuzi ifanyike kabla ya 2022.
 
Wanasiasa wanaomuunga Dkt Ruto wanasema hawapingi referenda kabla ya 2022 bali wanachotaka ni mdahalo unaofaa kuhusu kura hiyo.
Mnamo Jumamosi, Bw Odinga alipuuza miito ya kufanya kura ya maamuzi 2022 akisema mipango ya kuiandaa kabla ya uchaguzi mkuu imeshika kasi na haiwezi kusimamishwa.
Alisema kwamba referenda itafanyika hata kama baadhi ya watu hawataki kwa sababu ni Wakenya walioomba ifanyike.
“Wakenya wataamua ikiwa wanataka referenda, lakini ninaweza kuwahakikishia kwamba itafanyika. Ni Wakenya watakaoamua wanachotaka katika kura hiyo,” akasema.
Bw Odinga alisema yeye na Rais Uhuru Kenyatta wanasubiri kupokea ripoti ya kamati ya Mpango wa Maridhiano (BBI), kabla ya kuanza awamu ya pili ya kuhamasisha umma kuhusu mapendekezo ya ripoti hiyo na umuhimu wa mpango huo.
Wandani wa Dkt Ruto ambao wamekuwa wakisema referenda inafaa kufanyika pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022 ili kupunguza gharama jana walilegeza msimamo na kusema hawaipingi mradi tu imeidhinishwa na Rais Kenyatta.
Kulingana na mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali, ambaye ni mtetezi sugu wa Dkt Ruto, referenda haitafanyika kwa sababu Bw Odinga alisema itafanyika lakini itategemea iwapo Rais Kenyatta ataidhinisha ifanyike.
“Referenda ni hadithi ndefu ambayo itategemea uamuzi wa rais na sio wa Bw Odinga, hii ndiyo sababu ODM ilitaka isimamie kamati ya bunge kuhusu sheria na ikipitishwa katika kamati, itawasilishwa bungeni na tukiibadilisha bungeni itaenda kwa Rais ambaye atairudisha bungeni, na amini, ikiwa Rais anataka ifanyike itafanyika tu,” alisema Bw Washiali.
Akihutubia taifa wakati wa maadhimisho ya siku kuu ya Madaraka Dei mwaka huu, Rais Kenyatta alisema anaona huu ukiwa wakati wa kurekebisha katiba.
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa na mwenzake wa Keiyo Kusini Daniel Rono ambao pia ni wandani wa Dkt Ruto waliambia Taifa Leo kwamba, wanategemea nyadhifa zitakazobuniwa kupitia kura ya maamuzi ili waweze kuongea na viongozi wengine kubuni muungano wa kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2022.
“Hatuna shida na itakapofanyika mradi tu mtu atakayeunda serikali ijayo atachaguliwa kwa wingi wa kura, huu ndio msimamo wetu,” alisema Bw Barasa.
Mbunge huyo aliongeza kuwa wapinzani wao wa siasa hawako tayari kuzungumza nao kuhusu mahitaji ya nchi wakati huu watu wengi wanahangaika kutokana na janga la corona.
Alisema licha ya Bw Odinga kusema kwamba referenda itafanyika wapende wasipende, hawapingi mageuzi ya katiba yatakayobuni nyadhifa nyingi za uongozi serikalini.
Kulingana na Bw Rono, kambi ya Dkt Ruto iko tayari kwa kura ya maamuzi hata kama ingefanyika leo lakini kinachowapa wasiwasi ni janga la corona linalofanya Wakenya kuteseka.
“Dai la Bw Odinga kwamba referenda itagharimu Sh2 bilioni ni ndoto tu lakini ikiwa pesa ziko basi wailete, tuko tayari lakini kama wanaweza kusubiri hadi baada ya janga la corona itakuwa bora zaidi,” alisema.

You can share this post!

EUROPA LEAGUE: Sevilla yanyamazisha Manchester United

ULIMBWENDE: Unaweza kutumia tangawizi kukuza nywele zako