• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kashfa ya vyama kadha kusajili raia kwa lazima yakera Wakenya wengi

Kashfa ya vyama kadha kusajili raia kwa lazima yakera Wakenya wengi

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA wamelalamika kuwa vyama vya kisiasa nchini vimekuwa vikitumia ukora kuwasajili kuwa wanachama bila idhini yao.

Tangu Ijumaa, Wakenya wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuelezea ghadhabu yao baada ya kubaini kwamba, wao ni wanachama wa vyama mbalimbali vya kisiasa bila wao kujua.

Maelfu ya Wakenya wanasema wamesajiliwa kwenye vyama wasivyovijua na wala hawajawahi kuvisikia.

Kuna vyama 80 vya kisiasa vilivyosajiliwa nchini Kenya na asilimia kubwa havijulikani na havina hata kiongozi mmoja aliyechaguliwa.

Takwimu za Msajili wa Vyama vya Kisiasa zinaonyesha kuwa, Wakenya milioni 16.3 wamejisajili kuwa wanachama wa vyama mbalimbali vya kisiasa nchini.

Msajili wa Vyama Vya Kisiasa Ann Nderitu anasema idadi ya Wakenya wanaosajiliwa imeongezeka ndani ya miezi minane iliyopita. Hata hivyo idadi kubwa ya Wakenya walisema kwamba, wamegudua walisajiliwa na vyama vya kisiasa kwa njia ya mkato bila wao kujua.

Hii inaonyesha huenda vyama vya kisiasa vimekuwa vikitumia ujanja kupata rekodi zilizo na taarifa za watu kwa njia haramu kwa mfano kutoka kwa wahudumu fisadi wa maduka ya Mpesa.

Miongoni mwa waliojipata wamesajiliwa katika vyama vya kisiasa bila idhini yao ni mwanawe kiongozi wa ODM Raila Odinga, Junior, ambaye rekodi za Msajili wa Vyama vya Kisiasa zinaonyesha kuwa ni mwanachama wa Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi.

“Ni nini kinaendelea hapa?” akauliza Bw Raila Odinga Junior baada ya rekodi kuonyesha kuwa ni mwanachama wa ANC.

Bw Godwins Rapudo, mtumiaji wa mtandao wa Twitter, anasema alijipata akiwa mwanachama wa United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu wa Rais William Ruto, bila kujua.

Naye Matilda Otuma anasema hakifahamu chama cha Liberal Democratic Party ambacho rekodi zinaonyesha kuwa yeye ni mwanachama wake.

You can share this post!

UHURU AFYEKEA RAILA NJIA

Kamati yaonya Knec kuhusu jengo lililokwama