• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Kingi ashangazwa na mienendo ya Uhuru

Kingi ashangazwa na mienendo ya Uhuru

NA MAUREEN ONGALA

SPIKA wa bunge la Seneti Amason Kingi amemkosoa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa kujitokeza hadharani kutangamana na viongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya wakiongozwa na Raila Odinga aliyeitisha maandamano.

“Tulitarajia kwamba Rais mstaafu Uhuru Kenyatta angekuwa mstari wa mbele kumpa sapoti Rais William Ruto lakini anahujumu bidii za rais wetu. Hastahili kuihujumu serikali ambayo aliikabidhi mamlaka,” akasema spika Kingi ambaye ni gavana wa zamani wa Kaunti ya Kilifi alipokuwa akihutubu Ijumaa katika uwanja wa Karisa Maitha.

Spika Kingi amepuuzilia mbali wito wa Rais William Ruto ambaye mapema wiki hii aliashiria kwamba yuko tayari kukaa na kufanya mazungumzo na Bw Odinga.

Kulingana na Bw Kingi, majadiliano hayo hayatateremsha bei za vyakula nchini.

“Leo hii Rais Ruto akimuita Bw Odinga wakae pamoja, baada ya mkutano ule bei za vyakula zitakuwa ni zile zile,” akasema.

Spika huyo anasema suluhu ya tatizo la kupanda kwa gharama ya maisha sio mazungimzo baina ya Rais Ruto na Bw Odinga bali ni serikali ya Kenya Kwanza kutekeleza manifesto yake.

“Hata rais Ruto awe na mikutano mingapi na Bw Odinga, bei ya unga haitashuka. Lakini ile siku Wakenya watampa Rais Ruto nafasi atekeleze manifesto yake bei za bidhaa nyingi zitaanza kushuka,” akaeleza huku akijitetea kwamba aliamua kuwahepa viongozi hao alipong’amua walishindwa kuwatetea Wakenya mwaka 2022.

“Nilikuwa abiria wa mwisho kushuka katika meli hiyo iliyokuwa inazama kwa hivyo najua mengi yaliyofanywa kule. Wale ambao wanasema maisha yamepanda walikuwepo wakati ule, yale mawazo mazuri mazuri ambayo wanasema wanataka kukaa kwa meza ili wampatie Rais Ruto atekeleze, walikuwa wapi wakati bei ya unga ilikuwa tayari iko juu?” akauliza.

Kinara huyo wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA), aligura kutoka kwa mrengo wa Azimio dakika za mwisho mwaka 2022 na kujiunga na Kenya Kwanza.

Hii ni baada ya Kingi kudai kuwa Bw Odinga hakuwa tayari kuyatatua matakwa ya Wapwani haswa dhuluma za kihistoria za ardhi, ugavi wa keki ya serikali kuu na tatizo la ugavi wa nafasi za kazi katika serikali ya kitaifa.

Alihama Azimo miezi michache kuelekea uchaguzi.

Alisema maandamano yasiyo na mpangilio ni ya kufedhehesha na yanaletea Kenya aibu kubwa.

“Baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, viongozi wa upinzani walichukua hatua ya kwenda kortini kutafuta haki na mahakama ya upeo ilitoa uamuzi kwamba aliyechaguliwa na Wakenya kisheria ni Rais William Ruto,” akasema.

Alimtaka gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro kutokubali maandamano katika kaunti hiyo na kumuonya kuwa sio kati ya mizani itakayotumika na wakazi wa Kilifi kuamua utendakazi wake.

“Mwaka 2027 hawa wakazi wa Kilifi hawawezi kukuchagua kulingana na idadi ya maandamano uliyoleta Kilifi. Watakuchagua kulingana na idadi ya hatimiliki ulizowapa wananchi, hospitali ulizojenga na jinsi ulivyowasaidia wavuvi,” akasema.

Alisema kuwa sekta ya utalii imeathirika pakubwa kufatia maandamano yanayoendelea kupangwa na upinzani na kuathiri mwananchi wa kawaida.

“Watalii wengi wamefutilia ziara zao na hawatakuja tena hapa Kilifi. Hasara inaenda kwa watu wetu ambao wanategemea utalii,” akasema.

Alimwambia gavana Mung’aro kuwa ataweza kutimiza malengo yake kwa wakazi wa Kilifi endapo atafanya kazi na serikali kuu.

“Rais ana uwezo mkubwa wa kukushika mkono na kukuelekeza uwe wa manufaa kwa wakazi wa Kilifi,” akasema.

Aliwataka Wakenya kutojihusisha na maandamano.

“Hakuna faida kwa hayo maandamano yasiyo na mpangilio bali hasara tupu,” akasema.

Aidha, spika Kingi alieleza kushangazwa kwake kwamba gavana wa Kilifi anapanga mikakati ya namna ya kuwavutia watalii huku kinara wa chama chake cha ODM akiitisha maandamano yanayowafukuza wawekezaji wa sekta ya utalii na watalii wenyewe.

“Hatujui utafanyaje, lakini kwa sababu ulichaguliwa na chama cha ODM, Bw Odinga akiwekwa hapa na wananchi hapo, simama na watu wako,” akashauri.

  • Tags

You can share this post!

Miss Independents watoa Sh300,000 wapachikwe mimba

Azimio wakubali mazungumzo ya maridhiano na KK

T L