• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Kingi kuingia Azimio kupitia lango la Jubilee

Kingi kuingia Azimio kupitia lango la Jubilee

NA MARY WANGARI

CHAMA cha Gavana wa Kilifi, Amason Kingi sasa kimeweka rasmi hatima yake mikononi mwa Rais Uhuru Kenyatta baada ya kutia saini muafaka wa kujiunga na chama cha Jubilee.

Pan African Alliance (PAA) inayoongozwa na Gavana Kingi ni miongoni mwa vyama vitatu vilivyojiunga jana na Jubilee pamoja na chama cha Union Party cha Gavana wa Nyamira, Amos Nyaribo na United Progressive Alliance (UPA) kinachoongozwa na Gavana wa Pokot Magharibi, John Lonyangapou.

Akizungumza Ijumaa, Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju alisema vyama hivyo vitatu sasa vitawakilishwa na Rais Uhuru Kenyatta wakati wa mazungumzo na muungano mkuu wa Azimio la Umoja.

Bw Tuju alifichua kuwa Jubilee inatarajiwa vilevile kutia saini mkataba na vyama vingine vitatu ikiwemo PNU, DAP-K na UDM kabla ya Kongamano lake la Kitaifa la Wajumbe (NDC) litakalofanyika leo Jumamosi utakaoviwezesha kujiunga rasmi na Muungano wa Azimio la Umoja.

“Hii leo Februari 25, 2022, PAA pamoja na vyama vinginevyo vya kisiasa vyenye mtazamo sawa imetia saini mkataba wa ushirikiano na Chama cha Jubilee. Lengo la muafaka wa ushirikiano ambao PAA imetia saini leo ni kutoa nafasi kwa mchakato wa mazungumzo ya kina yatakayowezesha kutia saini Mkataba wa Kabla ya Uchaguzi,” ilisema taarifa kutoka kwa Gavana Kingi.

Kulingana na Gavana wa Kilifi, mkataba huo wa Ushirikiano umeipa PAA fursa ya kushiriki kwenye meza ya kitaifa ya majadiliano.

“Mkataba huu umepatia PAA fursa ya kuwakilisha kwenye meza ya kitaifa ya majadiliano masuala matatu makuu ambayo PAA inapigia debe. Masuala haya ni: suala lililodumu kwa muda mrefu kuhusu ardhi, uchumi wa pwani na ujumuishaji katika serikali kuu,” akasema.

“Mara tu itakapoafikiana, PAA itatia saini Mkataba wa Kabla ya Uchaguzi na vyama vingine vya kisiasa vyenye mawazo sawia chini ya Muungano wa Azimio,” alifafanua Bw Kingi.

Hatua hiyo ya Bw Kingi imejiri siku moja tu baada ya kiongozi wa Chama cha Party of National Unity (PNU), Waziri Peter Munya kufichua kuwa chama chake kimefanya mkataba na Rais Kenyatta ambaye atatetea maslahi yake kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Waziri huyo alisema haya katika kongamano la NDC la PNU lilioandaliwa katika Ukumbi wa Bomas na uliohudhuriwa na kiongozi wa ODM, Bw Odinga aliyeombwa kumteua Bw Munya kuwa mgombea mwenza wake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya aliyekuwa waziri mkuu, Ndiritu Muriithi alieleza Taifa Leo kuwa viongozi wa vyama vilivyokubali kuunga mkono azma ya urais ya Bw Odinga watatarajiwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Azimio la Umoja.

Gavana huyo wa Laikipia, hata hivyo hakuthibitisha iwapo Rais Kenyatta atahudhuria mkutano huo wa Kamukunji ulioahirishwa au la.

Akihutubu katika ikulu ndogo ya Sagana, Kaunti ya Laikipia, Jumatano, Kiongozi wa Taifa alialika vyama vidogo katika eneo la Mlima Kenya kujiunga na Azimio la Umoja.

You can share this post!

Raila apata tikiti ODM kuwania urais mara 5

TUSIJE TUKASAHAU: Jubilee na ODM havijafanya chaguzi za...

T L