• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Kiongozi mwenye nia njema afaa kurithi mikoba ya Rais Kenyatta, asema waziri Macharia

Kiongozi mwenye nia njema afaa kurithi mikoba ya Rais Kenyatta, asema waziri Macharia

Na MWANGI MUIRURI

KWA muda sasa, mrengo wa ‘Tangatanga’ unaoongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto umekuwa ukitoa malalamishi kwamba mtandao ulio na nguvu kupindukia ndani ya serikali almaarufu Deep State umekuwa ukipanga njama ya kushawishi matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Wiki jana, nao wakereketwa wa kiongozi wa ODM Raila Odinga wakatangaza kwamba kulikuwa na njama hiyo na wakamtaja Katibu maalum wa Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho kama aliyekuwa mshukiwa wa kushawishi matokeo hayo.

Aidha, kupitia wandani wa Bw Odinga ambao ni Seneta James Orengo na mbunge Junet Mohammed, ODM ilisema njama hiyo pia inalenga kuteka nyara mradi wa maridhiano ya kitaifa kupitia BBI.

Serikali haijakuwa ikijibu lakini Alhamisi katika Kaunti ya Murang’a, Dkt Matiang’i alihitilafiana hadharani na Waziri wa Uchukuzi James Macharia kuhusu njama hiyo.

Dkt Matiang’i na Bw Macharia walikuwa wameandamana na mwenzao wa Habari na Teknolojia Joe Mucheru katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Murang’a ambapo walifungua afisi za kiusalama Kirwara, Gatura, Kariara, Kigumo na wakatembelea Shule ya Upili ya Njiiri ambapo walitoa Sh500,000 ili wanafunzi 1,904 wanaosomea hapo waandaliwe mlo spesheli.

Jioni watatu hao wakafungua mradi wa ujenzi wa soko la kisasa mjini Kangari ambao utagharimu Sh320 milioni.

Huku Dkt Matiang’i akikanusha kwa ukali wote wa wizara yake ambayo ndiyo hifadhi kuu ya bunduki, risasi, pingu na vitoa machozi, Bw Macharia alisema madai hayo “yana ukweli.”

Dkt Matiang’i alisema kuwa hakuna wakati wowote serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imekuwa ikijiingiza katika siasa za mapema.

“Rais amekuwa muwazi kwamba kwanza tutekelezee wananchi maendeleo tukingoja wakati muafaka wa siasa ufike,” akasema Matiang’i.

Waziri huyu ambaye huonekana kupendelewa sana kwa njia ya kipekee na Rais Kenyatta kiasi cha kubandikwa jina la majazi la “Super CS”, alisisitiza kuwa “kuna wale ambao wameamua kazi yao ni siasa kila kuchao.”

“Sisi ndani ya serikali tunashughulika na masuala nyeti ya kuinua hali ya maisha ya Wakenya,” akaeleza.

Alichukua fursa hiyo kumkashifu Dkt Ruto ambaye amekuwa akitoa malalamiko katika mikutano ya hadhara kuwa Inspekta Mkuu wa Polisi Bw Hillary Mutyambai amekuwa akichokora siasa za ‘Tangatanga’ kwa nia ya kuhujumu uwezo wa kuwania 2022.

Wandani wake wa ‘Tangatanga’ wakikamatwa kuhusu madai mbalimbali, Dkt Ruto husisitiza wanateswa kwa msingi wa kuwa wafuasi wake wa kisiasa, akilimbikizia lawama zote Bw Mutyambai.

“Kuna mambo ambayo mimi sijawahi kuyawaazia kuwa yangenikumba katika uhai huu wangu na mojawapo wa hayo ni kujidunisha kujibu upuzi. Lakini huyu mtu (Dkt Ruto) yuko katika kamati moja ya usalama wa kitaifa (NSC) na Bw Mutyambai na sioni haki ya kwenda kwa matanga na mazishi kumzomea hadharani,” akasema Dkt Matiang’i.

Alisema kuwa Dkt Ruto angekuwa muungwana na mustaarabu, angekuwa akimsakama Bw Mutyambai kwa njia rasmi “lakini sio kumgeuza vibonde katika hafla za mazishi na matanga.”

Lakini wakati Bw Macharia alisimama kuongea, alifichua kuwa “baada ya Rais Kenyatta kustaafu 2022, baadhi yetu sisi ndani ya serikali tumeamua kuwa ni lazima aliye na maono mema ya taifa hili achukue usukani.”

Alisema kuwa serikali kwa sasa inaendeleza miradi tele kote nchini na ambayo ni ya mabilioni ya pesa hivyo basi kuiweka katika hatari ya kukwama iwapo asiye na maono mema ya taifa hili ataibuka rais baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Sisi tukiwa marafiki wa Rais tumezingatia mengi ya kutufaa kama taifa na tumeafikiana kwamba aliye na hayo maono sio mwingine bali ni Dkt Matiang’i,” akasema Dkt Macharia.

Bw Macharia alisema umefika wakati ambapo “hatuwezi tukanyamaza tena kuhusu hili.”

“Tupigwe vita vya kisiasa au tukemewe, tuko tayari na tumeamua na tumeingia katika ile awamu ambayo hatuna aibu wala hofu ya kutangaza hilo hadharani,” akaeleza waziri Macharia.

Dkt Matiang’i aliposimama kuongea, alikwepa kukubali mwito huo wa kuwania urais 2022 na badala yake akaelezea watu wa Mlima Kenya jinsi walivyo na “bahati ya mtende ya kuwa na kinara wa siasa (rais Kenyatta) ambaye kando na kuwajali kisiasa, pia anawalilia kirasilimali.”

Aliwataka wenyeji wa Mlima Kenya wazingatie umoja nyuma ya rais Kenyatta na wasusie siasa za mapema hasa zile za ghasia na “mtii Rais kuletea wananchi maendeleo kwanza na hatimaye awaongoze katika kusaka mstakabali wa kisiasa kuongoza urithi wa Ikulu 2022.”

Eneo la Kati limekuwa liking’ang’aniwa kisiasa na Rais Kenyatta na Naibu wake na hadi sasa hakujabainika waziwazi kati yao wawili ni nani ana ushawishi mkuu miongoni mwa wapigakura hao ambao wanakisiwa kuwa 8 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Tottenham sasa guu moja ndani ya robo-fainali za Europa...

Roma, Villarreal na Ajax waweka hai matumaini ya kufuzu kwa...