• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
Miguna aahidi kuzima ufisadi Nairobi

Miguna aahidi kuzima ufisadi Nairobi

Na CHARLES WASONGA

MWANASHERIA mbishani anayeishi uhamishoni Miguna Miguna ametangaza kuwa atawania kiti cha ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Februari 18.

Akijipigia debe kwenye mahojiano na runinga ya Diaspora TV, Dkt Miguna anayeishi nchini Canada aliahidi kuleta mabadiliko makubwa katika uongozi wa kaunti ya Nairobi kwa manufaa ya wakazi wa jiji.

“Nawasalimu nyote watu wa Nairobi na Wakenya kwa ujumla. Huyu ni Jenerali Miguna akiongea akiwa uhamishoni. Nitagombea nafasi ya ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mdogo ujao,” akasema.

“Nitatokomeza ufisadi, na kuteleta mabadiliko katika jiji kwa kuendeleza uongozi wenye maadili,” akaongeza kwenye mohajiano hayo ambayo video yake ilisambazwa mitandaoni.

Hata hivyo, Bw Miguna Miguna ambaye amezuiwa mara kadha kurejea nchini kwa madai kuwa hana stakabadhi hitajika, hakuelezea ikiwa atakubali kutii masharti ya idara ya uhamiaji ili aweze kurejea Kenya kwa ajili ya kushiriki uchaguzi huo.

Vile vile, haikujulikana ni vipi ahatakikisha kuwa stakabadhi zake za uteuzi zimefikia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ikiwa serikali itaendelea kumzuia kuingia nchini.

Mwanasheria huyo ana uraia wa Cananda japo ni raia wa Kenya kwa misingi ya kuzaliwa Kenya. Hata hivyo, jaribio lake la kurejelea Kenya mapema 2019 liligonga mwamba alipodinda kujaza stakabadhi hitajika ili kurejesha uraia wake wa Kenya.

Miguna Miguna alifurushwa nchini kwa kosa la kuongoza kiapo bandia ya kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Januari 31, 2018 kuwa “Rais wa Wananchi” katika hafla iliyofanyika katika bustani ya Uhuru, Nairobi.

Mapema Jumatatu, Desemba 28, 2020 ilidaiwa kuwa chama cha Thirdway Alliance kimemdhamini kuwa mgombeaji wake katika kinyang’anyiro hicho.

Hata hivyo, barua ambayo ilifichua habari hizo na ambayo ilidaiwa kuandikwa na mwenyekiti wa chama hicho Miruru Waweru ilibainika kuwa feki.

You can share this post!

NCIC yasema haitawashtaki Sifuna na Jumwa

Afiza wa zamani wa KDF asema polisi walitaka kumtia adabu