• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Mikakati ya Uhuru ‘kukomboa’ Mlima

Mikakati ya Uhuru ‘kukomboa’ Mlima

NA MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta ameweka mikakati thabiti ‘chini ya maji’ kuhakikisha kwamba amelinasua eneo la Mlima Kenya kutoka mikononi mwa chama cha UDA cha Naibu Rais William Ruto.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhakikisha kuwa chama chake cha Jubilee kimeshinda viti visivyopungua 80 vya ugavana, useneta, wabunge na wawakilishi wa kike katika kaunti za Mlima Kenya.

Washirika wa Dkt Ruto katika Mlima Kenya wamekuwa wakijigamba kuwa umaarufu wa UDA ni thabiti katika eneo hilo ambalo limekuwa ngome ya chama cha Jubilee.

Wakosoaji wa Rais wanasema kwamba anataka Jubilee kuwa chama cha Mlima Kenya ili kimsaidie kubaki katika siasa kwa madhumuni ya kulinda maslahi yake ya kibinafsi na ya washirika wake wasio wanasiasa. Hata hivyo, washirika wake wanasema kwamba ana mipango mizuri kwa ngome yake ya Mlima Kenya.

Kulingana na wanaomuunga mkono, kuendelea kuwa msemaji wa Mlima Kenya na kujadiliana kwa niaba ya eneo hilo katika serikali ijayo, Rais Kenyatta atafaulu tu chama chake kikiwa na wabunge, magavana, maseneta na wawakilishi wengi wa kike. Hii itampa ushawishi mkubwa kwa rais atakayemrithi na kudhibiti eneo hilo kwa kuwa na usemi katika chaguzi za urais siku zijazo.

Huku Rais akiunga azma ya urais ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kupitia muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Dkt Ruto atapeperusha bendera ya UDA, chama ambacho wadadisi wanasema kimepata umaarufu mkuu eneo la Mlima Kenya.

“Rais ametuamuru tuondoke katika ofisi zetu, tuache kukutana kwenye kumbi na katika hoteli, kwamba mkakati wa kujadili siasa tukinywa na kula umepita, akisisitiza ni wakati wa kuingia mashinani kufanya kampeni kali,” alisema Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni.

Alisema awamu ya kupanga uchaguzi na kufufua chama imepita na sasa ni wakati wa kutambua wawaniaji maarufu Nairobi, Nakuru, Nyandarua, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nyeri, Embu, Meru, Tharaka Nithi na Laikipia, mkakati ambao umekaribia kukamilika.

Alisema awamu inayofuata ni kupigia debe chama na wagombeaji wake. Aliyekuwa mgombeaji urais, Peter Kenneth anasema Jubilee inalenga kushinda viti 50 vya ubunge.

“Tukifaulu kushinda viti 11 vya ugavana na idadi sawa na hiyo ya maseneta na wawakilishi wa kike, na tuongeze wabunge wasiopungua 50, tutakuwa sawa, rais wetu atakuwa akiongoza kikosi imara na atakuwa akizungumza moja kwa moja na Rais Odinga,” akasema.

Mbunge wa Gatanga, Nduati Ngugi anasema kuna sababu muhimu ambayo inamfanya Rais Kenyatta kutaka Mlima Kenya kuungana ndani ya Jubilee.

“Ni kuhusu kutambuliwa kama eneo letu. Rais anawekeza rasilmali nyingi na msaada wa kitaalamu kufanya Jubilee kuwa chama chenye nguvu katika utawala ujao,” akasema Bw Nduati.

Rais Kenyatta amekuwa akikutana na wadau muhimu katika siasa za Mlima Kenya kisiri na amewapa majukumu kadhaa kukabili wimbi la UDA,” alisema mdhamini wa kitaifa wa Baraza la Wazee wa Jamii la Agikuyu, Ndung’u Gaithuma.

“Rais amekuwa na shughuli nyingi chini ya maji kukutana na wadau tofauti wa eneo la Mlima Kenya ambao watatekeleza jukumu muhimu kusaidia kuzima tatizo la UDA miongoni mwa watu wetu,” alisema.

“Tayari tuna viongozi wa kidini tuliobadilisha, vyama vya wataalamu, wazee, wanasiasa waaminifu, vikundi mbali mbali na wafanyabiashara,” aliongeza.

Aliyekuwa mbunge wa Molo Njenga Mungai alisema mikakati ya Rais Kenyatta kuzima wimbi la Hasla la Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya ni thabiti.

  • Tags

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Njaa: Serikali imewasahau wakazi wa...

Chelsea wadengua Palace na kujikatia tiketi ya kuvaana na...

T L