• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Mradi wa Uhuru 2022

Mradi wa Uhuru 2022

NA JUSTUS OCHIENG

MMOJA kati ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Seneta Gideon Moi wa Baringo, atakuwa mradi wa Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi wa urais mwaka ujao.

Taifa Leo imebaini kuwa marafiki wakuu wa Rais Kenyatta wakiongozwa na David Murathe wanampendelea Bw Odinga. Kwa upande mwingine, kuna kundi la washirika wakuu wa rais wanaoshirikisha watu wa familia yake ya Kenyatta, ambao roho zao zipo kwa Bw Moi.

Duru zingine zinadokeza kuwa kuna wandani wa Rais Kenyatta ambao wanapendelea tiketi ya pamoja ya Bw Odinga kama mwaniaji urais na Bw Moi akiwa naibu wake.

Juhudi hizo zimejitokeza kwenye msururu wa mikutano, wa kwanza ukiwa wa Aprili 13 wakati nduguye rais, Muhoho Kenyatta alipokutana na wawili hao nyumbani kwa Bw Odinga.

Juhudi hizo pia zimekuwa zikifanywa na marafiki wa Bw Odinga na Bw Moi, ambapo tayari wameandaa mikutano miwili nyumbani kwa rafiki wa karibu wa Kiongozi wa ODM katika Kaunti ya Siaya.

Mikutano hiyo, duru zimesema, inakusudiwa pia kutafuta uwezekano wa kubuni muungano mkubwa unaoshirikisha vigogo wengine wa siasa isipokuwa Naibu Rais William Ruto.

Mikutano hiyo imekuwa ikifanyka nyumbani kwa mfanyibiashara Edwin Ng’ong’a kingoni mwa Ziwa Kanyaboli, eneo la Usoga, ambayo ilihudhuriwa na Bw Moi na washirika wake.

Baadhi ya walio karibu na wawili hao wanasema suala la kuunganisha Bw Odinga na wenzake katika Muungano wa One Kenya Alliance unaoshirikisha Bw Moi, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka na Moses Wetang’ula linajadiliwa kwa makini.

Katibu Mkuu wa Kanu, Nick Salat alithibitisha kufanyika kwa mikutano hiyo, na kuwa alihudhuria mmoja kati ya miwili iliyofanyika pamoja Bw Moi pamoja na Mbunge wa Tiaty, William Kamket.

“Ni kweli tumekutana nyumbani kwa Bw Ng’ong’a, lakini sikuwepo kwenye kikao cha Jumapili iliyopita, ingawa Bw Moi alikuwepo,” akasema Bw Salat.

Hapo jana, Bw Mudavadi alikiri kuwepo kwa juhudi za kupanua muungano wao wa OKA ili kushirikisha watu zaidi kabla ya uchaguzi mwaka ujao.

“Gideon na timu yake wamekuwa wakikutana nyumbani kwa Bw Ng’onga eneo la Alego na Naivasha wakiwa na baraka za Bw Odinga,” akasema mmoja wa marafiki wa mfanyibiashara huyo.

Nduguye Bw Odinga, Oburu Odinga alikiri kuwa ODM inajaribu kushawishi viongozi wa OKA kufanya kazi nao, lakini akasisitiza sharti wawe tayari kumuachia Bw Odinga kuwania urais.

“Ni wazi kuwa Bw Odinga hawezi kutaka cheo cha waziri mkuu kwa sababu amewahi kukalia kiti hicho. Ni urais pekee ambao hatujawahi kupata na hapo ndipo macho yetu yamelenga,” akasema Bw Oburu.

Kulingana na Seneta Enoch Wambua wa Kitui, majadiliano yanayoendelea ya kubuni muungano mkubwa kwa ajili ya 2022 ndiyo yaliyomshawishi kupiga kura ya “Ndio” kwa Mswada wa BBI, licha yake kuupinga awali.

Bw Wambua alisema Bw Musyoka alimwambia kuwa kuna mashauriano yanayoendelea katika ngazi ya kitaifa kuhusu uongozi wa nchi, na kuwa kura yake dhidi ya BBI ingeharibu nafasi ya Wakamba kwenye majadiliano hayo.

Wengine wanaotajwa kushirikishwa kwenye muungano huo unaoungwa mkono na Rais Kenyatta ni nduguye Muhoho, Mukhisa Kituyi, Peter Kenneth na magavana Alfred Mutua (Machakos), Hassan Joho (Mombasa), Charity Ngilu (Kitui) na Anne Waiguru (Kirinyaga).

Hata hivyo, juhudi za kubuniwa kwa muungano mkubwa zimezua kiwewe miongoni mwa washirika wa muda mrefu wa Bw Odinga, ambao wanahisi huenda wakapoteza ushawishi wao kwa Bw Odinga.

You can share this post!

Liverpool waadhibu Man-United ugani Old Trafford

Ruto alenga waasi wa Odinga Luo Nyanza