• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Liverpool waadhibu Man-United ugani Old Trafford

Liverpool waadhibu Man-United ugani Old Trafford

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Jurgen Klopp alisherehekea ushindi wake wa kwanza ugani Old Trafford kwa kuwaongoza Liverpool kutoka nyuma na kuwacharaza Manchester United 4-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoimarisha nafasi yao ya kucheza soka ya bara Ulaya muhula ujao.

Mechi hiyo ilisakatwa wakati ambapo mashabiki wa Man-United walikuwa wamekongamana nje ya uwanja wa Old Trafford wakiandamana kwa mara nyingine kulalamikia hatua ya wamiliki wa Man-United kuingiza kikosi hicho kwenye kipute kipya kilichosambaratika cha European Super League (ESL).

Mojawapo ya mabasi ya Liverpool yaliyokuwa yakisafirisha wachezaji hadi ugani Old Trafford lilizuiliwa na mashabiki waliokuwa wakiandamana.

Kiungo Bruno Fernandes aliwaweka Man-United kifua mbele katika dakika ya 10 kabla ya Diogo Jota kusawazisha mambo katika dakika ya 34.

Roberto Firmino, aliyekuwa amefunga bao moja pekee tangu acheke na nyavu mara mbili dhidi ya Crystal Palace mnamo Disemba 2020, aliwaweka waajiri wake kifua mbele mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya kufunga goli la tatu la Liverpool katika dakika ya 47.

Marcus Rashford alifunga bao la pili la Man-United katika dakika ya 68 kabla ya fowadi Mohamed Salah kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili. Bao la Salah lilikuwa lake la 21 katika EPL kufikia sasa msimu huu wa 2020-21.

Idadi ya mabao ya Salah sasa inawiana na ile inayojivuniwa na fowadi Harry Kane wa Tottenham Hotspur ambaye pia anafukuzia fursa ya kutawazwa Mfungaji Bora wa EPL msimu huu. Mechi dhidi ya Liverpool ilikuwa ya sita kwa Man-United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer kupoteza katika kampeni za msimu huu.

Japo Man-United wanasalia katika nafasi ya pili jedwalini kwa alama 70, Liverpool kwa saasa wanashikilia nafasi ya tano kwa pointi 60. Man-United watacheza na Fulham ugani Old Trafford katika mechi yao ijayo huku Liverpool wakiwaendea West Bromwich Albion mnamo Mei 16, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Real Madrid yapepeta Granada na kuendeleza presha kwa...

Mradi wa Uhuru 2022