• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Mung’aro abanwa kuhusu uteuzi wa mwaniaji mwenza

Mung’aro abanwa kuhusu uteuzi wa mwaniaji mwenza

MAUREEN ONGALA NA ALEX KALAMA

ALIYEKUWA Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, anakabiliwa na changamoto ya kuamua atakayekuwa mgombea mwenza wake wa ugavana Kaunti ya Kilifi katika uchaguzi wa Agosti.

Hii ni baada ya makundi tofauti ya kisiasa na kijamii kumshinikiza kuchagua watu tofauti, huku wanawake wakimtaka kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, amwagize kumchagua mwanamke.

Miongoni mwa wale wanaotajwa ili wachaguliwe kupewa nafasi ya mgombea-mwenza ni Naibu Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Saburi, Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi, Bw Jimmy Kahindi, na Bi Winnie Chivila.

Bi Chivila awali alitaka kuwania ubunge wa Kaloleni kupitia ODM kabla ya chama hicho kumkabidhi mbunge wa sasa, Bw Paul Katana tikiti ya moja kwa moja.

Kabla mwanasiasa huyo kuanza kupendekezwa, makundi ya wanawake yalikuwa yanampigia debe Bi Jane Kamto kuwa mgombea mwenza wa Bw Mung’aro.

Bi Kamto ni dada yake naibu gavana wa Kilifi wa zamani, marehemu Kenneth Kamto.

Bw Mung’aro anatarajiwa kuweka kwenye mizani masuala kama vile kabila la mgombea mwenza, tajriba yake ya uongozi na kisiasa, na uwezo wake wa kuvutia idadi kubwa ya kura uchaguzini.

Wanaompigia debe Bw Saburi kupewa nafasi hiyo walisema mbali na kuwa atawakilisha maslahi ya jamii ya Warabai katika serikali ya kaunti, naibu gavana huyo amedhihirisha uwezo wake wa uongozi katika utawala wa gavana anayeondoka, Bw Amason Kingi.

“Kwa sababu yeye alikuwa anaendea ugavana lakini akakubali kumwachia Bw Mung’aro kwa ajili ya umoja wa chama, ana haki ya kuwa naibu gavana. Ana ujuzi na tajiriba na sisi tunamuunga mkono na sio Rabai peke yake. Hao wengine waliopendekezwa ni limbukeni katika mambo haya ya uongozi wa kaunti,” akasema kiongozi wa kijamii, Bw Abdalla Shakalo, akiandamana na wenzake.

Duru zilisema, Bw Kahindi ni miongoni mwa walio katika nafasi kubwa ya kutangazwa mgombea mwenza wa Bw Mung’aro hivi karibuni.

Hata hivyo, juhudi za kumfikia Bw Mung’aro ili athibitishe mpango wa kumchagua Bw Kahindi hazikufua dafu kufikia wakati wa gazeti hili kuchapishwa.

Spika huyo wa bunge la kaunti pia alikuwa akitaka tikiti ya ODM kuwania ugavana kabla ya chama hicho kinachoongozwa na Bw Odinga kuamua kura ya mchujo haingefanyika.

Bw Kahindi pia alikuwa akipinga uamuzi wa chama kutoa tikiti ya moja kwa moja.Kwa upande mwingine, makundi ya wanawake wa ODM na wawaniaji huru wanaounga mkono muungano wa Azimio la Umoja One Kenya katika Kaunti ya Kilifi, wametishia kususia uchaguzi iwapo mgombea mwenza wa ugavana hatakuwa mwanamke.

Wanawake hao wanataka Bi Chavila ndiye awe mgombea mwenza wa Bw Mung’aro.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa kikundi cha wanachama wa kike wa ODM katika kaunti hiyo, Bi Barkhe Mohamed, walisisitiza wanawake pia wanao uwezo wa kuwa viongozi bora iwapo watapewa nafasi.

“Wanawake wamekosa viti vingi kwa kupigwa vita na wanaume kisiasa. Kama wanawake wamenyimwa nafasi ya kutuwakilisha mashinani, watupe unaibu ugavana. Tuko na wamama ambao na tajriba ya kuongoza,” akasema.

Bi Chivila alisema ilishangaza jinsi ODM ilivyoteua mwanamke mmoja pekee kuwania ubunge kaunti hiyo, katika eneobunge la Malindi.

Alitoa wito kwa chama hicho kusawazisha hali iliyopo ya uwakilishi wa kijinsia kwa kuhakikisha nafasi ya mgombea mwenza wa ugavana inaendea mwanamke.

  • Tags

You can share this post!

Faini ya Sh30,000 kwa kuharibu kifaa cha umeme

Conde hatimaye afunguliwa mashtaka

T L