• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Muturi ataka kamati ichunguze dai ardhi ya wakazi ilinyakuliwa

Muturi ataka kamati ichunguze dai ardhi ya wakazi ilinyakuliwa

Na ANITA CHEPKOECH

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ameamuru kamati ya bunge hilo kuhusu ardhi kuchunguza madai ya kufurushwa kwa familia kadhaa kutoka ardhi ya ekari 8,500 na kugeuzwa mashamba ya majani chai katika kaunti ya Bomet.

Hii inafuatia malalamishi ya watu wa baadhi ya familia hizo wanaodai kuwa walipokonywa ardhi hiyo iliyoko katika eneo la Kimulot mnamo 1952 na kampuni ya kigeni ya James Finlays inayoendesha kilimo cha majani chai eneo hilo.

Familia za Kipsoi araap Chemoroe na Tapsimate arap Borowo zilisema ardhi yao ilitwaliwa kwa upanuzi wa mashamba ya majani chai ya kampuni ilijulikana kama African Highlands Tea Company, nyakati hizi ikijulikana kama James Finlay.

Walalamishi hao wanalitaka Bunge la Kitaifa kuwasaidia warejeshewe ardhi yao ambayo sasa imepandwa zao hilo na kujengwa viwanda vitatu.

“Afisi yangu imepokea malalamishi kutoka kwa wawakilishi wa familia za Araap Borowo na Arap Chemorore, ambao ni marehemu, kuhusu dhuluma za kihistoria kuhusu ardhi zilizotendewa wakazi wa eneo la Kimulot.

“Familia hizo ambazo zinaishi sasa katika kaunti za Bomet na Kericho zinadai kuponyokwa ardhi yao na serikali wa kikoloni kati ya 1948 na 1953,” Bw Muturi akasema Ijumaa, akirejea hati hiyo yenye malamishi.

Watu wa familia hizo wanadai kuwa mnamo Agosti 1, 1951, Serikali ya Ukoloni wa Uingereza iliipa kampuni ya Kimulot Tea Company, sasa ikijulikana kama James Finlay (Kenya) Ltd, idhini ya kutumia ardhi hiyo kwa miaka 999 bila.

Serikali hiyo haikusaka idhini ya wenye ardhi hiyo wala kuwalipa fidia yoyote.

Ardhi hiyo inajumuisha vipande mbalimbali vilivyopokonywa wakazi na kusajiliwa kwa namba LR no 8804 yenye ukubwa wa takriban ekari 4,500.

Hatua hiyo ilichangia wakazi hao kuondolewa kutoka ardhi ya mababu zao.

Vipande vingine vya ardhi hiyo vinapatikana katika maeneo ya Kerenga, Chebown na Timbili (Magharibi mwa Msitu wa Mau).

Walalamishi hao wanasema wazee hao wawili walikataa kuondoka katika ardhi hiyo kwa hiari hali iliyopelekewa wao kufurushwa kwa nguvu.

Mnamo Machi mwaka huu Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) ilitoa uamuzi kwamba wakazi wote katika kaunti za Bomet, Kericho na Nandi ambao ardhi zao zilitwaliwa kwa upanzi wa majani chai warejeshewe.

  • Tags

You can share this post!

Mahabusu waliotoroka wakanusha shtaka

Kenya yadumisha nafasi yake kwenye kamati ya Wake wa Marais...

adminleo