• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Nassir: Sonko na Omar hawanitishi

Nassir: Sonko na Omar hawanitishi

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, amepuuzilia mbali hatua ya wapinzani wake kuungana dhidi yake katika kinyang’anyiro cha ugavana Mombasa.

Bw Nassir, anayewania ugavana kupitia Chama cha ODM, amesema hababaishwi na jinsi aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, ameamua kuunga mkono azma ya aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, kushindania kiti hicho.

Bw Omar anawania kiti hicho kupitia Chama cha UDA.Kulingana na mbunge huyo, tangazo la Bw Sonko kwamba wameweka maelewano kuhusu watakavyogawana nafasi za mamlaka katika serikali ya kaunti, ni ishara inayoonyesha hawana ajenda ya kutumikia wananchi.

Bw Sonko alikuwa amedai kuwa amehakikishiwa nafasi tatu za uwaziri na tatu za maafisa wakuu wa kaunti, endapo Bw Omar atafanikiwa kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho katika Uchaguzi Mkuu wa wiki ijayo.

“Mombasa haiko sokoni kuuzwa. Mimi sitaweka mkataba wowote aina hiyo na mtu binafsi. Kuna watu washanikujia wakitaka niwaahidi nafasi za kisiasa ili waniunge mkono lakini mkataba wangu ni kati yangu na watu wa Mombasa pekee. Hata wakiungana kivipi hawatashinda uchaguzini. Ninataka kuwaambia wale ambao wameshinda wakinitusi, mimi ndiye nitakuwa gavana wao,” akasema Bw Nassir.

Mgombea mwenza wa mbunge huyo, Bw Francis Thoya, alitoa wito kwa wakazi kujitenga na viongozi wanaotaka kuwagawanya kwa misingi ya kikabila.

Maafisa wa Chama cha Wiper katika Kaunti ya Mombasa, wamesema hatua ya Bw Sonko ilikuwa ya usaliti kwao.

Wiper inayoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais, Bw Kalonzo Musyoka, ilikuwa imempa mwanasiasa huyo tikiti ya moja kwa moja kuwania nafasi hiyo.

Awali, tikiti hiyo ilikuwa imetarajiwa kumwendea Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, lakini akashawishiwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko.

Hata hivyo, juhudi nyingi za Bw Sonko kutaka kuwania kiti hicho licha ya kuwa alitemwa mamlakani Nairobi baada ya bunge la kaunti hiyo na seneti kumpata na hatia za ufisadi na ukosefu wa uadilifu, ziligonga mwamba.

Mwenyekiti wa Wiper katika Kaunti ya Mombasa, Sheikh Omar Twaha, alisema Wiper haitamfuata Bw Sonko katika Kenya Kwanza bali itaunga mkono Bw Nassir chini ya chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

“Wakati huo wote alikuwa anamuunga mkono Bw Ruto na UDA lakini sasa amejitokeza wazi. Tunamtakia kila la heri,” akasema Bw Twaha.

Alisema pigo pekee wanalosikitikia katika Wiper, ni kwamba hawatakuwa na mgombeaji ugavana.

Nafasi ambayo jopo la kutatua mizozo ya uchaguzi katika IEBC ilipatia chama hicho kuteua mgombeaji mwingine awali, ilishapitwa na muda.

Chama hicho sasa kinajaribu kumshawishi Bw Mbogo asalie upande wao, huku kikimlaumu Bw Sonko kwa kumharibia mipango yake ya kisiasa.

“Tunatumai Bw Mbogo atabaki katika Wiper lakini akiamua kuungana na gavana wa zamani wa Nairobi, tutamtakia kila la heri,” akasema.

Viongozi wa jamii ya Wakamba, wakiongozwa na Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu, pia walipuuzilia mbali hatua ya Bw Sonko.

Akizungumza katika eneo la Changamwe, Bi Ngilu alisema jamii hiyo itasimama wima kumuunga mkono Bw Nassir.

  • Tags

You can share this post!

Gavana apigia debe ukuzaji wa vipaji kuzima maovu ya vijana

WANTO WARUI: KNEC isahihishe dosari katika usajili wa...

T L