• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Ngoma ya BBI itarindima tena – Joho

Ngoma ya BBI itarindima tena – Joho

BRIAN WACHIRA na VALENTINE OBARA

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho ameeleza matumaini kuwa mswada wa kurekebisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) utapita licha ya kuharamishwa na mahakama kuu.

Akizungumza Jumatano mjini Mombasa, Bw Joho alitabiri kuwa ngoma ya BBI itarejelewa hivi karibuni na atakuwa tena mstari wa mbele kuisakata.

“Bado mimi nina matumaini BBI itapita. Wakati ukifika utatuona tukivaa mabuti, tutakutana mashinani tu,” akasema.

Kulingana na Bw Joho, kuharamishwa kwa BBI ni pigo kwa Kaunti ya Mombasa kimaendeleo.

Alisema kuwa, endapo mswada huo utapitishwa katika kura ya maamuzi, Kaunti ya Mombasa itaongezewa maeneobunge matatu.Kwa msingi huu, anaamini pesa za Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) zingeongezeka.

“Kitovu cha maendeleo mashinani ni maeneobunge. Watu wanaangalia tu ongezeko la wawakilishi bungeni lakini hapa Mombasa tungepata Sh390 milioni zaidi kupitia maeneobunge mapya matatu,” akasema.

Vile vile, alisema mpango wa kuongeza mgao wa fedha za serikali za kaunti ungewezesha Mombasa kuongeza mgao wake kutoka Sh6 bilioni hadi Sh12 bilioni.

Majaji watano wa mahakama kuu waliamua kwamba mchakato wa kutaka kurekebisha katiba ulikiuka sheria zilizopo.Hata hivyo, watetezi wa mpango huo wanataka Mahakama ya Rufaa ibatilishe uamuzi huo wakisema una dosari.

  • Tags

You can share this post!

Kamket ataka apewe maelezo kuhusu aliko Spika Muturi na...

Maafisa wa DCI wakita kambi Kilifi kupeleleza serikali ya...