• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
ODM yaanza kufuta nyayo za UDA Nyanza

ODM yaanza kufuta nyayo za UDA Nyanza

NA GEORGE ODIWUOR

CHAMA cha ODM kimeanza kuwakusanya wafuasi wake kukabili uvamizi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika Kaunti ya Homa Bay.

ODM imewaagiza wafuasi wake katika kaunti hiyo kuhakikisha wametumia kila mbinu kuhakikisha wamedhibiti mafanikio ambayo UDA imepata katika eneo hilo kwa miezi michache iliyopita.

Hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kupunguza juhudi za Rais William Ruto kupenya kisiasa katika eneo la Nyanza.

Eneo hilo, ambalo ni ngome ya kisiasa ya kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga, limekuwa likishambuliwa na wanasiasa kutoka mrengo wa Kenya Kwanza.

Mnamo Ijumaa, viongozi wa kamati shirikishi ya ODM walifanya kikao maalum wakiongozwa na mwenyekiti wa chama katika kaunti hiyo, Bi Gladys Wanga, na katibu, Bw Ong’ondo Were, ambapo walijadili mikakati ya kukiboresha chama.

Bi Wanga alisema kwamba lengo kuu la mkutano huo ni kufufua umaarufu wa chama hicho katika mashinani na ngazi ya kitaifa.

“Sisi ndio chama kikubwa zaidi cha kisiasa nchini na hii ni ngome ya ODM. Tumekuja pamoja ili kujadiliana kuhusu mikakati ya kukiboresha chama kwani tumejitolea kumuunga mkono kiongozi wake,” akasema Bi Wanga, ambaye ndiye gavana wa kaunti hiyo.

Naibu Gavana wa Homa Bay Oyugi Magwanga, wabunge Lilian Gogo (Rangwe), Eve Obara (Kabondo Kasipul), Adipo Okuome (Karchuonyo) ni miongoni mwa wale waliohudhuria mkutano huo.

Spika wa Bunge la Kaunti Julius Gaya pia aliwaongoza madiwani kadhaa kuhudhuria mkutano huo.

Viongozi hao walikubaliana kwa pamoja kusukuma mbele mikakati ya chama hicho pamoja.

Kwenye maamuzi yaliyowasilishwa kwa Bi Wanga, chama hicho kiliamua kwamba kitahakikisha kitakuwa na afisi yake katika kila wadi.

Walisema kuwa hilo litahakikisha chama kina mwonekano katika kila sehemu kaunti hiyo.

Madiwani walipewa jukumu la kuhakikisha kuwa afisi hizo zinaendeleza shguhuli zake kama kawaida.

“Nawarai viongozi kutembelea afisi hizo mara nyingi ili kuhakikisha zinaendelea na shughuli zake kama kawaida. Lazima afisi zote katika kiwango cha kaunti ziwe zikiendelea na shughuli zake kuanzia Desemba 1,” akasema Bi Wanga.

Kulingana na gavana huyo, chama hicho kitajenga afisi zake katika kaunti, ambako shughuli zake zote zitaendeshwa huko.

Aliwahakikishia wanachama kuwa jengo la afisi hiyo litakuwa limekamilika kufikia Aprili 2024.

  • Tags

You can share this post!

Wanakriketi wa Nairobi kutuzwa kwa mara ya kwanza na NPCA...

Wanahabari wapewa ujuzi wa masuala muhimu ya kidijitali

T L