• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
ODM yazidisha wito Ruto ajiuzulu enzini

ODM yazidisha wito Ruto ajiuzulu enzini

RUSHDIE OUDIA na ANGELINE OCHIENG

WANDANI wa kiongozi wa ODM Raila Odinga wameendelea kutoa shinikizo kwa Naibu wa Rais William Ruto kujiuzulu kwa madai ya kupinga Rais Uhuru Kenyatta.

Mbunge wa Rarieda Dkt Otiende Amollo na mwenzake wa Gem Elisha Odhiambo na Askofu wa Kanisa la Anglikana Profesa David Kodia, pia walimtaka Dkt Ruto kutangaza mali yake yote.

Walimtetea waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i dhidi ya madai kwamba anatumiwa kusambaratisha ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu mwaka 2022.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakishutumu Dkt Matiang’i kwa kufichua kuwa Naibu wa Rais analindwa na jumla ya maafisa wa polisi 257.

“Usilaumu Waziri Matiang’i kwa kufichua utajiri wako. Ikiwa unahisi kwamba alitoa taarifa ya uongo kuhusiana na mali yako, usitueleze. Anika wazi kiasi cha fedha ulizo nazo kwenye akaunti za benki na mashamba unayomiliki ili Wakenya wajiamulie wenyewe,” akasema Dkt Amollo.

Viongozi hao waliokuwa wakizungumza Jumamosi mazishini katika eneo la Chianda, Rarieda, Kaunti ya Siaya, walimtaka Dkt Ruto kujiuzulu ikiwa anahisi kwamba serikali inayoongozwa na Rais Kenyatta imeshindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi.

“Ruto hafai kuendelea kukosoa serikali ya Jubilee ilhali yeye ni sehemu ya serikali. Ajiuzulu ili akosoe serikali akiwa nje,” akasema Dkt Amollo.

Mbunge wa Gem Bw Odhiambo alitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kuchunguza mali ya Dkt Ruto na kunasa aliyojipatia kwa njia isiyofaa.

“Wakenya wanafaa kuwa na wasiwasi, mtu kujiita mlala hoi ilhali anamiliki zaidi ya ekari 10,000 huko Laikipia na ekari 2,500 katika eneo la Voi,” akasema Bw Odhiambo.

Askofu Kodia alisema kuwa Dkt Ruto amekuwa katika siasa tangu alipokuwa kijana na kuna uwezekano alijipatia mashamba hayo makubwa kutokana na ushawishi wake serikalini.

“Inashangaza kuwa muda ambao amekuwa serikalini amefanikiwa kulimbikiza mali ya mabilioni ya fedha. Amevunja rekodi na anafaa kuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha Guiness kwa kuwa mwanasiasa wa kwanza kugeuka bilionea ndani ya kipindi kifupi,” akasema.

Askofu Kodia aliwataka Wakenya kukemea wanasiasa ambao wamejitajirisha kwa mali ya wizi.

Wanasiasa hao pia walisema kuwa rufaa ambayo imewasilishwa katika Mahakama ya Juu katika juhudi za kutaka kuokoa Mswada wa Marekebisho ya Katiba (BBI) haina uhusiano na kiongozi wao Bw Raila Odinga.

“Raila hajakata rufaa, sisi mawakili wake tumemshauri aachane na BBI na badala yake ajishughulishe na kampeni za kwenda Ikulu,” akasema Dkt Amollo.

You can share this post!

Makanisa yakataa Ruto

MMUST: Viongozi Magharibi wapuuza habari za kupotosha...