• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Pigo kwa Chris Wamalwa kambi ya Natembeya ikipigwa jeki

Pigo kwa Chris Wamalwa kambi ya Natembeya ikipigwa jeki

NA GERALD BWISA

MBUNGE wa Kiminini Chris Wamalwa anayewania kiti cha ugavana Trans Nzoia amepata pigo, baada ya mmoja wa waliokuwa wakiwania wadhifa huo na wandani wake watatu kuhamia mrengo wa mpinzani wake mkuu, Bw George Natembeya.

Bw Philemon Samoei ambaye alikuwa akiwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), Kipkoech Arap Mutai, Julian Kichwen na Teresa Metto walitangaza kuwa watamuunga mkono Bw Natembeya.

Watatu hao walitoa tangazo hilo katika kituo cha Ukombozi Centre mjini Kitale wakati ambapo Dkt Wamalwa alikuwa akimzindua mgombea mwenza wake – Bethwel Kirior – katika uwanja wa AIC Chebarus Ijumaa jioni.

Bw Kirior ambaye ni mwalimu mkuu wa zamani katika shule ya upili atashirikiana na Dkt Wamalwa kushindania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Ford Kenya.

Bw Samoei ambaye ni mwanajeshi aliyestaafu, alinyimwa tiketi ya UDA kuwania kiti hicho cha ugavana wa Trans Nzoia baada ya muungano wa Kenya Kwanza kuamua kuunga mkono azma ya Dkt Wamalwa.

Mnamo Ijumaa, Bw Samoei alisema anaunga mkono sera na maongozi ya Bw Natembeya ambaye anawania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Democratic Action Party (DAP-K).

“Leo ni furaha yangu kujiunga na ndugu yangu Natembeya. Silalamiki kutokana na kile ambacho kilinitendekea, lakini baada ya kutafakari kwa undani nimeng’amua kuwa ninaunga mkono sera zake,” akasema.

Bi Metto, ambaye awali alionyesha nia ya kuwania ugavana lakini akaamua kusaka nafasi ya naibu gavana baada ya UDA kubuni muungano na Ford Kenya na ANC, alielezea kukerwa na hatua ya Dkt Wamalwa kuteua mgombea mwenza wake bila kufanya mashauriano.

“Tulikubaliana na Wamalwa kwamba atenge nafasi hiyo kwa jamii ya Nandi lakini badala yake akafanya uamuzi wake binafsi kumteua Bw Kirior,” akasema.

Wakiongea na wanahabari katika kituo cha kushirikisha kampeni za Bw Natembeya, ambaye zamani alihudumu kama Mratibu wa Rift Valley, wanne hao waliusuta muungano wa Kenya Kwanza kwa kutojumuisha wanawake katika nafasi za uongozi.

Kwa upande wake, Bw Natembeya aliwahakikishia viongozi hao kwamba serikali yake itashirikisha watu kutoka jamii zote.

“Tunawakaribisha wale wote ambao wameamua kufanya kazi nasi. Mimi ni mradi wa wananchi na ninataka kutoa huduma zangu kwa wananchi. Lengo langu si mamlaka tu,” akasema.

Bw Natembeya mnamo Jumatano Mei 25 anatarajiwa kumzindua Bi Philomena Bineah Kapkory kama mgombea mwenza wake. Shughuli hiyo itafanyika katika mkahawa Mt Elgon Lounge ulioko eneo la Kokwo katika eneobunge la Endebess.

  • Tags

You can share this post!

Walimu waunga azma ya Wanga kuwania ugavana

Man-City wakomoa Aston Villa ugani Etihad na kuhifadhi taji...

T L