• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Polisi watishia kuzima kampeni Nyali baada ya fujo

Polisi watishia kuzima kampeni Nyali baada ya fujo

WINNIE ATIENO NA KEVIN ODIT

POLISI katika Kaunti ya Mombasa, wameonya watazima kampeni zote za kisiasa eneobunge la Nyali iwapo wanasiasa hawatakomesha vurugu.

Kumekuwa na makabiliano kati ya pande tofauti za kisiasa katika siku za hivi majuzi, ambapo idadi isiyojulikana ya vijana walijeruhiwa.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Bw John Otieno, alisema idara ya usalama haiwezi kukaa kimya wakati vijana wanaendelea kuchochewa kuzua vurugu kabla ya uchaguzi.

Alikuwa akizungumza Jumapili, baada ya kukutana na Mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali, anayewania kiti hicho kwa tikiti ya Chama cha UDA, na mpinzani wake, Bw Said Abdalla (ODM), ambao inaaminika vijana wanaozozana ni wafuasi wao.

“Tutaendeleza uchunguzi kikamilifu na yeyote ambaye atapatikana na hatia, ataadhibiwa kisheria,” akasema.

Usalama umeimarishwa katika eneobunge hilo na imebainika kumetumwa maafisa zaidi wa kikosi cha GSU ili kuzima fujo zozote zinazoweza kutokea.

Mkutano huo wa Jumapili ulihudhuriwa pia na afisa mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Kaunti ya Mombasa, Bi Swalhah Ibrahim.

Bi Ibrahim aliwataka wanasiasa wajitolee kueneza amani wakati huu ambapo imesalia siku chache kabla Uchaguzi Mkuu ufanywe.

Awali, wagombeaji hao wawili wa ubunge walikuwa wamejitenga na vurumai ambazo zilisababishia vijana walioaminika kuwa wafuasi wao majeraha, ambapo baadhi yao walilazimika kulazwa hospitalini.Walikana kuhusika na vurugu hizo wakisisitiza wanataka kampeni za amani zidumu.

Vijana hao walivamiana walipokuwa katika harakati za kutangaza sera za wagombeaji hao wawili mitaani.Walioshuhudia kisa hicho waliiambia Taifa Leo kuwa walirushiana mawe na kujeruhiana.

Eneobunge la Nyali ni mojawapo ya yale ambayo yanaaminika kuwa na ushindani mkali kati ya ODM na UDA.

Chama cha ODM kilipoteza eneobunge hilo katika Uchaguzi Mkuu uliopita, wakati Bw Ali aliposhinda akiwa mgombeaji huru.

  • Tags

You can share this post!

Mgombeaji wa ugavana Kilifi ajiondoa na kuunga mkono Kithi

Gavana apigia debe ukuzaji wa vipaji kuzima maovu ya vijana

T L