• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
Raila motoni kwa kumgonga Kingi

Raila motoni kwa kumgonga Kingi

NA WINNIE ATIENO

VIONGOZI wa mrengo wa Kenya Kwanza eneo la Pwani wamemshtumu mwaniaji wa urais wa muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga kwa kumlaani Gavana wa Kilifi Amason Kingi kwa kukihama chama chake cha ODM.

Walisema Gavana Kingi ana uhuru wa kuchagua chama anachokitaka.

Kwenye ziara yake ya Pwani, Bw Odinga alimsuta gavana Kingi na mwenzake wa Kwale Bw Salim Mvurya kwa kushirikiana na mpinzani wake wa kisiasa Dkt William Ruto.

“Nilimpata amemaliza shule nikamfanya waziri wa mambo ya Afrika Mashariki na hata uvuvi kwa sababu bahari iko hapa, mwaka wa 2013 nikarudi Kilifi nikampigia debe awe gavana kila sehemu akapita na kura nyingi. Mwaka 2017 nikampigia debe na akapita akawa na matatizo akakimbia kwangu nikamsaidia, lakini kuanzia mwaka jana akaanza kubadilika,” alisema Bw Odinga.

Bw Odinga alisema Bw Kingi alimwambia Wapwani hawataki ODM na angependelea kuunda chama cha Wapwani.

“Nikajaribu kuzungumza naye nikiwa na Bw Joho akakataa, Bw Kingi hana adabu, amenipiga teke ya punda, asante ya punda ni mateke. Nataka nyinyi wapiga kura mumpige teke kwa niaba yangu ili ajue chuma chake ki motoni,” alisema Bw Odinga hapo juzi kwenye kampeni huko Kilifi.

Hata hivyo, viongozi wa Pwani wakiongozwa na wabunge Mohammed Ali, aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar na Gavana Kingi wamemshtumu Bw Odinga kwa kumkashifu kiongozi huyo.

Bw Kingi alijiondoa kutoka muungano wa Azimio One Kenya na kuhama chama ODM alichochaguliwa nacho katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017 kwa kile alichodai ni kukosekana kwa uwazi, heshima na uwiano.

“Tuko kwa hivi vita sababu tumedhulumiwa, twakata viwanda vya samaki, bandari yetu na kufufua uchumi wa Pwani,” alisema Bw Ali.

Gavana Kingi alisema hakumsaliti Bw Odinga bali yeye ndiye aliwasaliti wapwani kwa kuwanyima nafasi za uteuzi.

“Ulisaliti wapwani, ulikuwa wapi wakati kazi za Bandari zilipokuwa zikienda baada ya kuhamisha hadi Naivasha? Ulikuwa wapi wakati vijana wetu walikosa kazi Bandarini? Kilifi ndio kaunti pekee iliyotoa viti vingi vya ODM, chama cha Jubilee hata hakikupata kiti chochote lakini kilimteua mtoto wetu,” alisema Bw Kingi.

Gavana Kingi alisema Kilifi ilisimama kidete na kaunti hiyo lakini haikuzaidiwa.Alisema kaunti ya Kilfi iliambulia patupu kwenye chama cha ODM kwa kukosa uteuzi.

Bw Omar alisema kuingia kwa Gavana Kingi kwenye muungano wao kumepiga jeki Kenya Kwanza Alliance.

Walisema watashirikiana na wapwani wote na kufanya kampeni ili kuhakikisha wanamzolea Bw Ruto kura nyingi.

Bw Ali alisema pwani itanufaika kutokana na serikali ya Bw Ruto akisema wameahidiwa nafasi ikiwemo mawaziri na mabalozi katika nchi za Uarabuni.

Gavana Kingi alisema hajutii kujitoa katika mrengo wa Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wanafunzi wenye uhitaji wa kweli wa karo wasaidiwe

Baadhi ya Wazee wa Kaya waunga Sonko Mombasa

T L