• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
TAHARIRI: Wanafunzi wenye uhitaji wa kweli wa karo wasaidiwe

TAHARIRI: Wanafunzi wenye uhitaji wa kweli wa karo wasaidiwe

NA MHARIRI

UKARIMU wa Wakenya mara nyingi huonekana wakati wanafunzi wenye uhitaji wa karo ya shule hutakikana ili kufanikisha masomo yao. Hakika, kuna watoto wengi maskini ambao hawangejiunga na shule.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na taarifa za wanafunzi wa kidato cha kwanza kufika katika shule zao mpya wakiwa na masanduku matupu na barua zao za kujiunga na shule hizo pekee.

Wanafunzi hawa wanastahili kusaidiwa, kwa kuwa wamejitahidi sana kufaulu mtihani wao wa Cheti cha Elimu ya Msingi nchini (KCPE).

Tukio la kwanza liliwafanya watu wengi kutokwa na machozi na wengine walichanga fedha ili kuwezesha kijana huyo kupokelewa shuleni. Swali sasa ni iwapo baadhi ya wazazi wajanja wanaweza kuwa wakipanga njama ili kufaidika na hisani nzuri ya Wakenya.

Mwaka huu, kumekuwa na visa kadhaa vya vijana maskini wanaoripotiwa kutembea umbali mrefu au kukopa pesa kutoka kwa majirani na kupanda boda boda hadi shuleni kwao.

Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa ukarimu huu kutumiwa vibaya. Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (CDF) na basari nyinginezo kila mwaka zinahudumia maelfu ya wanafunzi wenye uhitaji.Usaidizi unaotolewa kwa wanafunzi hao aghalabu si endelevu, na huenda ukaendeleza tabia ya utegemezi na hata ukosefu wa uaminifu miongoni mwa wanajamii.

Kwa hiyo kuna haja ya kuwa na utaratibu mzuri ambapo watoto kutoka familia maskini wanaweza kusaidiwa zaidi ya CDF na mipango ya basari. Pia, michango inayoombwa kupitia kunadi huku ni lazima ihesabiwe ipasavyo.

Hii pia inazua swali kuhusu jukumu la mzazi. Watu hawawezi tu kuendelea kupata watoto na kutumaini kwamba mtu mwingine atawahudumia.

Wanapaswa kuomba msaada pale tu wanapokosa. Kuhimiza vijana kusema uwongo ili kupata usaidizi kunakuja kuwasumbua baadaye maishani. Ni wanafunzi tu wenye uhitaji wa kweli wanapaswa kufaidika na ukarimu huu.

You can share this post!

Kikundi cha wanajuakali Kiambu chafurahia pendekezo la Raila

Raila motoni kwa kumgonga Kingi

T L