• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Raila sasa adai Ruto ananunua wabunge

Raila sasa adai Ruto ananunua wabunge

BENSON MATHEKA Na WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja One-Kenya, Bw Raila Odinga wanaendelea kuvutana kuhusu uasi wa wabunge wa muungano wa upinzani walioamua kushirikiana na serikali.

Viongozi hao wawili wameongoza washirika wao kushikilia misimamo mikali kuhusu uamuzi wa wabunge hao; tisa wa ODM na 30 wa Jubilee walioalikwa Ikulu na kukata kauli kuunga ajenda ya serikali ya Rais Ruto bungeni.

Mvutano wa mirengo hiyo miwili unazidi huku Bunge likianza vikao kesho baada ya likizo ndefu ya tangu mwisho wa mwaka jana ambapo Kenya Kwanza inapigania kuwa na ubabe kufanikisha ajenda zake.

Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Busia jana Jumapili, Bw Odinga alisisitiza kuwa kuhama kwa wabunge wa Azimio hakutatisha mrengo wa upinzani ambao unaamini ulishinda uchaguzi.

“Ikiwa walishinda kihalali, mbona wanawinda wabunge wa Azimio. Wanapaswa kuwa na idadi kubwa ya wabunge ikiwa kweli walishinda,” Bw Odinga alihoji na kusisitiza kuwa ushindi wake uliibwa.

Bw Odinga alionekana kupuuza hatua ya wabunge hao akisema kwamba Katiba imepwapa raia nguvu zaidi kuliko za wabunge.

“Waende. Sisi tumesema tutakuja kwa wananchi ambao kikatiba, ndio wenye nguvu zaidi na kwa kuwa ndio walitupigia kura ambazo walitupokonya,” alisema.

Bw Odinga aliambia serikali kwamba “kuwanunua wabunge hakutatia hofu Azimio ili iache kushinikiza mageuzi katika mfumo wa uchaguzi ikiwemo uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)”.

Wabunge wa ODM Mark Nyamita (Uriri), Phelix Odiwuor Jalang’o ( Lang’ata), Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Ochieng (Gem), Caroli Omondi (Suba Kusini), Walter Owino ( Awendo), Paul Abuor (Rongo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda wanadai walienda Ikulu kwa kuwa wanataka maendeleo katika maeneo yao, madai ambayo Bw Odinga amepuuza.

Akihutubu jana Jumapili akiwa Kaunti ya Nakuru, Rais Ruto alisema atafanya kazi na viongozi wote waliochaguliwa na wananchi.

Aliwataja wabunge ‘waasi’ wa Jubilee kuwa ‘wabunge wake’, kwani walichaguliwa kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 kabla ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kubuni handisheki.

“Mimi mwenyewe ndiye niliyewaalika wabunge wa Jubilee katika kikao hiki. Sababu kuu ni kuwa hawa ni wabunge tuliochaguliwa kwa chama kimoja kabla ya umoja tuliokuwa nao kuvurugwa na salamu (handisheki). Hivyo, sisi tu nyumba na familia moja,” akasema Rais Ruto.

Aliwarai wabunge hao pamoja na wale wa ODM ambao walimtembelea katika Ikulu Jumanne wiki iliyopita kutotishika hata kidogo kwa kushirikiana naye, akisema yuko tayari kuwapa mafunzo kuhusu “njia za kukabili vitisho hivyo”

“Nimepitia njia mliyopo kwa sasa. Mnamo 2013, mimi pamoja na Bw Kenyatta tulishiriki katika uchaguzi wa urais chini ya mazingira magumu sana. Wazungu na mataifa ya kigeni yalikuwa yametoa kila aina ya vitisho kwa Wakenya dhidi ya kutuchagua. Licha ya maonyo hayo, tuliibuka washindi kwa neema ya Mungu. Imani iyo hiyo ndiyo ilituwezesha kushinda uchaguzi wa 2017 na hatimaye 2022. Hivyo, msitishike hata kidogo,” akasema Rais Ruto.

Baadhi ya wabunge ‘waasi’ wa Jubilee waliokuwa katika kikao hicho ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Kanini Keega, Mbunge Maalum Sabina Chege, wabunge Kwenya Thuku (Kinangop) kati ya wengine.

Mnamo Ijumaa, Bw Kenyatta alitoa onyo kwa wabunge hao, akiwaambia kuondoka katika chama hicho baada ya kutangaza kumwondoa Katibu Mkuu Jeremiah Kioni na Naibu Mwenyekiti David Murathe na badala yake kuwateua Bw Keega kama Kaimu Katibu Mkuu, mbunge Rachael Nyamai (Kaimu Mwekahazina) na Adan Keynan kama Kaimu Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa.

Waziri mkuu huyo wa zamani alitaka hatua ya IEBC ya kutochapisha matokeo ya maeneo bunge ya uchaguzi uliopita kama ya kuficha ukweli usijulikane.

“Kufikia sasa, IEBC haijachapisha matokeo kutoka maeneo bunge 290 inavyohitaji katiba kwa sababu wanajua walivyofanya,” akasema na kuongeza kuwa njia ya pekee ya kupinga ripoti waliyohusisha na mfichuzi ni kufungua sava za IEBC.

Bw Odinga anasisitiza kuwa kulingana na ripoti hiyo ambayo imepandisha joto la kisiasa nchini, alishinda kura ya urais kwa zaid ya kura 8.1 milioni dhidi ya 5.7 milioni za Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Leicester wadhalilisha Tottenham katika EPL uwanjani King...

Pasta kutembea 237km kutoka Mtito Andei kumpa Ruto ujumbe...

T L