• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Rais anasa samaki wakuu katika ODM

Rais anasa samaki wakuu katika ODM

ONYANGO K’ONYANGO na LEONARD ONYANGO

RAIS William Ruto amechukua hatua za kupasua chama cha ODM katika juhudi za kulemaza kisiasa kinara wa chama hicho Raila Odinga.

Mgawanyiko ndani ya chama hicho cha Chungwa ulijitokeza wazi jana baada ya wabunge wanane wa ODM na kutoka ngome ya kisiasa ya kiongozi huyo wa upinzani ya Luo Nyanza kukutana na Rais Ruto pamoja na naibu wake Rigathi Gachagua katika Ikulu ya Nairobi.

Wabunge waliokutana na Rais Ruto ni Gideon Ochando (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Shakeel Shabir (Kisumu Mashariki), Felix Odiwuor maarufu Jalang’o (Lang’ata), Paul Abuor (Rongo) na Seneta wa Kisumu Prof Tom Ojienda.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Waziri wa Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) Eliud Owalo na Katibu wa Wizara ya Usalama Dkt Raymond Omollo.

Baadhi ya wabunge waliokutana na Rais Ruto wamekuwa wakikwepa mikutano ya kisiasa ambayo imekuwa ikiandaliwa na Bw Odinga kupinga serikali ya Kenya Kwanza.

Rais Ruto aliahidi kushirikiana na viongozi hao licha ya Bw Odinga kupinga serikali kwa kuandaa mikutano ya kisiasa.

Wabunge hao walipokuwa Ikulu, mwenyekiti wa ODM John Mbadi alikuwa katika kituo cha redio cha Nam Lolwe ambapo alijitenga na ripoti ya ufichuzi iliyodai kuwa Bw Odinga alishinda urais katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

“Sijui (Raila) alitoa wapi ripoti hiyo. Hajawahi kuketi na mimi kunielezea kwa mapana kuhusiana na ripoti hiyo. Siwezi kuzungumzia nisichokijua,” akasema Bw Mbadi.

Bw Odinga wiki iliyopita alidai kupokea ripoti ya ufichuzi kutoka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambapo alisema alishinda urais kwa zaidi ya kura milioni 8 huku Rais Ruto akifuatia kwa kura milioni 5.

Waziri Mkuu wa zamani anataka Rais Ruto kujiuzulu “kwa sababu hakuchaguliwa na Wakenya”. “Hatutambui serikali ya Kenya Kwanza, Rais Ruto na maafisa wa serikali,” akasema Bw Odinga.

Lakini jana Jumanne, Bw Mbadi alionekana kumponda Bw Odinga kwa kukanganya wafuasi wake.

“Rais Ruto alipozuru kaunti za Luo Nyanza, kiongozi wetu (Bw Odinga) alituhimiza kumpa mapokezi mema na kushirikiana naye kuleta maendeleo. Baadaye, tunaambiwa kuwa hatutambui serikali ya Rais Ruto huku ni kujikanganya,” akasema Bw Mbadi.

Katika mkutano wa jana Ikulu, viongozi wa Nyanza na ODM waliapa kuasi wito wa Raila wa kupinga serikali.
Rais Ruto aliambia viongozi hao wa Nyanza kuwa serikali yake haitabagua kimaendeleo eneo hilo licha ya Bw Odinga kuongoza maandamano dhidi ya serikali yake.

Rais Ruto alitumia mkutano huo kusihi wanasiasa wa Nyanza kuunga mkono ajenda ya serikali yake. Hatua ya Rais Ruto ‘kunyakua’ wabunge hao wa ODM italemaza zaidi upinzani Bungeni.

“Nataka kuwahakikishia Wakenya kwamba, mimi ni rais wa kila Mkenya bila kujali mirengo ya kisiasa. Tushirikiane ili tuunganishe nchi,” akasema Rais Ruto.

Wandani hao wa Bw Odinga, hata hivyo, waliambia Taifa Leo kuwa, waliamua kukutana na Rais Ruto ili kufahamu ikiwa mikutano ya Bw Odinga itaathiri miradi ya maendeleo ambayo kiongozi wa nchi aliahidi wakazi wa Nyanza alipozuru eneo hilo mwezi Januari.

“Tungali ndani ya ODM lakini tunahofia kuwa huenda serikali ikakataa kupeleka miradi ya maendeleo katika eneo la Nyanza. Rais ameahidi kushirikiana nasi katika kuendeleza ajenda ya serikali,” akasema Bw Ochanda.

Siasa za eneo la Luo Nyanza – linalojumuisha Kaunti za Migori, Homa Bay, Kisumu na Siaya – zimekuwa zikidhibitiwa na familia ya Odinga tangu Kenya kupata uhuru.

Eneo la Nyanza limeanza kuasi Bw Odinga baada yake kupoteza kura za urais mara tano. Umri wa Bw Odinga pia umechangia kwa viongozi wa Nyanza kumtoroka. Bw Odinga atakuwa na umri wa miaka 82 mnamo 2027 hivyo matumaini yake ya kushinda urais yamedidimia.

Viongozi wa Nyanza ambao wamekuwa wakitangaza kuunga mkono Rais Ruto wamekuwa wakionekana kujipanga nyuma ya Bw Owalo.

Rais Ruto anatarajiwa kuzuru Kaunti ya Migori mwezi ujao au mapema Aprili katika juhudi za kuendeleza ushawishi wake katika eneo la Luo Nyanza.

Rais Ruto jana Jumanne pia aliagiza naibu wake Bw Gachagua kukutana na mawaziri mbalimbali Jumatano ili kujadili mikakati ya kutekeleza miradi yote aliahidi wakazi wa Nyanza.

“Tutakutana na mawaziri mbalimbali chini ya uongozi wa Bw Gachagua kujadili jinsi ya kutekeleza ahadi zilizotolewa na Rais Ruto Nyanza,” akasema Bw Abuor.

“Uchaguzi umeisha; hatutaki kufanya siasa kila uchao. Tutafanyia kazi Wakenya wote,” akasema Dkt Ruto.

Chama cha ODM, hata hivyo, kilishutumu wabunge waliokutana na Rais Ruto ikulu kwa kuhujumu Bw Odinga.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ODM Philip Etale, chama hicho kilidai kuwa Rais Ruto amekuwa ‘akinunua’ wabunge wa Azimio.

Mwezi uliopita, Rais Ruto alikutana na baadhi ya wabunge wa Jubilee katika juhudi za kulemaza chama hicho kinachoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Wadadisi wanasema viongozi hao waasi huenda wakatumiwa na serikali kutekeleza ‘mapinduzi’ kwa kunyakua uongozi wa ODM na Jubilee na baadaye kuvipeleka katika muungano wa Kenya Kwanza.

Chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kimeanza harakati za kutaka kumeza vyama vilivyo ndani ya muungano wa Kenya Kwanza kikijiandaa kutetea urais 2027.

  • Tags

You can share this post!

Wizara ya Kilimo yapokea Sh650 milioni kama ruzuku kutoka...

Waliojenga madarasa ya CBC wasaka malipo miezi saba...

T L