• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 10:18 AM
Ruto amtaka Raila aeleze madai yake kwa uwazi zaidi

Ruto amtaka Raila aeleze madai yake kwa uwazi zaidi

NA WAANDISHI WETU

MAKABILIANO kati ya Rais William Ruto na kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, hayaonekani kuisha hivi karibuni, pande zote zikiendelea kurushiana cheche za maneno hadharani.

Majibizano kati ya Rais Ruto na Bw Odinga pamoja na wafuasi wao, yanazidi kutilia shaka uhuru wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika maandalizi ya uchaguzi mkuu uliopita.

Licha ya Dkt Ruto kutangazwa mshindi na IEBC, na matokeo hayo kuthibitishwa na Mahakama ya Juu ambapo Azimio ilikuwa imewasilisha malalamishi, mihemko ya kisiasa inayoendelea hasa tangu Bw Odinga aliporudi nchini kutoka Afrika Kusini wiki iliyopita, inaonyesha hali ambayo uhuru wa tume hiyo unashambuliwa kutoka pande zote.

Jana Jumatatu, Rais aliibua maswali kuhusu madai kwamba baadhi ya waliokuwa makamishna wa IEBC wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wao, Bw Wafula Chebukati, walimtembelea nyumbani kwake muda mfupi kabla ya uchaguzi huo kufanyika.

Bw Odinga alipohutubia mkutano wa hadhara Nairobi mnamo Jumapili, alitaka Bw Chebukati pamoja na waliokuwa makamishna, Prof Abdi Guliye, na Bw Boya Molu, waeleze wazi kwa nini walienda nyumbani kwake katika kipindi cha uchaguzi.

Alitishia kutoa hadharani video za CCTV anazodai ziliwanasa watatu hao wakiwa nyumbani kwake katika mtaa wa Karen.

Ni kufuatia madai hayo ambapo Dkt Ruto alipokuwa Mombasa jana Jumatatu alimtaka Bw Odinga atoe ufafanuzi.

Kulingana na Rais, haieleweki kwa nini madai hayo yametolewa wakati huu, na kwa nini Bw Odinga aliyekuwa mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo wa urais, alikubali kukutana na makamishna wa IEBC nyumbani kwake.

Vilevile, aliibua shaka kuhusu kwa nini hayo yote hayakusemwa wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika Mahakama ya Juu, kisha yanaenda kutangazwa katika mkutano wa hadhara.

“Jana (Jumapili) nilikuwa nasikiliza mmoja wa wanasiasa wetu akidai makamishna wa IEBC walienda nyumbani kwake, na anatoa habari hii miezi mitano baada ya tukio hilo na anajitolea kutoa habari hizi kwa sababu ambazo hajafichua,” akasema.

Rais alikuwa akizungumza alipofungua rasmi kongamano la Chama cha Viongozi wa Mashtaka barani Afrika, ambapo alisisitiza kuhusu umuhimu wa asasi huru za kitaifa kutoingiliwa na watu wenye ushawishi.

Alipuuzilia mbali dhana kuwa serikali yake inaingilia mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji, ikizingatiwa kuwa kesi nyingi zimefutiliwa mbali tangu alipoingia mamlakani.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Taifa, Bw Opiyo Wandayi, alisisitiza kuwa ni lazima sheria zinazosimamia IEBC zirekebishwe kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Akizungumza katika kongamano la wabunge lililoandaliwa na Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) mjini Mombasa, Bw Wandayi alisema uadilifu wa IEBC umetiliwa shaka kwa kiwango sawa na ilivyokuwa mwaka wa 2007.

“Huu mkutano hauwezi kuisha bila kujadili IEBC. Kuna shaka kuu kuhusu uwezo wa IEBC kusimamia uchaguzi wa uaminifu katika miaka ijayo. Tume ya uchaguzi lazima ifanyiwe marekebisho kwa njia tofauti,” akasema, huku akizomwa na wanasiasa wa Kenya Kwanza.

Mkutano huo wa wabunge pia ulifunguliwa rasmi na Dkt Ruto, ambaye alikuwa ameandamana na Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, na Kinara wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi.

Kiongozi wa wengi bungeni, Bw Kimani Ichung’wa, aliwarai wabunge kuweka kando tofauti zao za kisiasa kila wakati watakapohitajika kufanya maamuzi ambayo yatakuwa kwa manufaa ya taifa.

Bw Ichung’wa alisema bunge lina nafasi bora ya kuacha rekodi nzuri ya kutatua changamoto nyingi zinazokumba wananchi ikiwa maamuzi yatafanywa kwa njia ya busara bila kuwa na misimamo mikali ya kisiasa.

Ripoti za Winnie Atieno, Philip Muyanga na Valentine Obara

  • Tags

You can share this post!

Agizo la Gachagua kuhusu pombe halijatekelezwa

Kaunti ya Mombasa yalenga kuvuna zaidi kwa makongamano

T L