• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Ruto bado ni mchanga, amuunge mkono Raila, Waluke asema

Ruto bado ni mchanga, amuunge mkono Raila, Waluke asema

NA BRIAN OJAMAA

MBUNGE wa Sirisia, John Waluke, amemrai Naibu Rais William Ruto kuacha azma yake na urais na badala yake kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Alisema kuwa Dkt Ruto bado ni mchanga, hivyo anaweza kungoja hadi Bw Odinga amalize muhula wake ndipo apate nafasi ya kuwania urais.

Bw Waluke alikuwa mfuasi sugu wa Dkt Ruto kabla ya kuhama chama cha UDA mwezi uliopita na kujiunga na Jubilee.

“Dkt Ruto bado ni mchanga. Anaweza kungoja hadi pale Bw Odinga atamaliza muhula wake kuhudumu kama rais,” akasema Bw Waluke, alipohutubu katika kanisa la Sinoko PEFA, wadi ya Matulo, eneobunge la Webuye Magharibi, Kaunti ya Bungoma.

Alimtetea Bw Odinga, akisema ndiye atakayeibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti, huku akiwaomba wakazi wa Bungoma kumuunga mkono.

Alisema atatumia nguvu zake kuupigia debe muungano wa Azimio-One Kenya na kuendeleza ajenda ya maendeleo ya Bw Odinga katika eneo la Magharibi.

“Niliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuongoza kundi la Azimio katika eneo nzima la Magharibi. Ninaamini wakazi wengi wataunga mkono muungano huo,” akasema Bw Waluke.

Wakati huo huo, alimrai Spika wa Seneti Kenneth Lusaka kulenga nafasi kubwa zaidi kuliko kuwania ugavana katika Kaunti ya Bungoma.

Alisema kuwa nafasi yake ya Uspika katika Seneti imemweka katika nafasi ambapo anaweza kutafuta wadhifa mkubwa zaidi katika kiwango cha kitaifa, hivyo hapaswi kurejea katika siasa za kikanda.

“Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi analenga kuwa mgombea-mwenza. Mbona Bw Lusaka hafanyi hivyo?” akashangaa.

Aliwarai wenyeji kumpigia kura gavana wa sasa, Bw Wycliffe Wangamati ili kuhudumu kwa muhula wa pili.

Mbunge huyo alisema kuwa Bw Wangamati amefanya maendeleo makubwa ambayo yanaonekana na kila mmoja.

“Msidanganyike hata kidogo. Rekodi za maendeleo za Bw Wangamati na Spika Lusaka zinatofautiana sana. Nawaomba kufanya maamuzi ya busara kwa kumrejesha (Wangamati) kama gavana,” akasema.

Vile vile, aliwarai kumkataa kiongozi wa Ford-Kenya, Moses Wetangula kama seneta na badala yake kumchagua Bw Charles Ngome kama seneta mpya. Bw Ngome ndiye naibu gavana wa Bw Wangamati.

Akihutubu katika kanisa lilo hilo, Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa, alisema kuwa ameendesha miradi mingi ya maendeleo katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia tangu alipojiunga na serikali.

Bw Wamalwa alisema kuwa miradi mingi iliyo katika eneo hilo inatokana na juhudi zake.

“Viongozi walio katika muungano wa Kenya Kwanza wamekuwa wakiwadanganya kwamba sijafanya lolote,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

NCIC yashtakiwa kuhusu marufuku ya ‘Sipangwingwi’ na...

Wanabiashara wa miraa wakashifu serikali kwa kukosa...

T L