• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Ruto na Raila wazua vita kwa washirika wao

Ruto na Raila wazua vita kwa washirika wao

NA BENSON MATHEKA

WAGOMBEAJI wakuu wa urais katika uchaguzi mkuu ujao, Raila Odinga wa Azimio la Umoja-One Kenya na Naibu Rais William Ruto wa Kenya Kwanza, wamesababisha vita vya ubabe katika ngome za washirika wao kwa kuwaahidi nyadhifa za juu serikalini iwapo watashinda urais Agosti 9.

Katika eneo la Ukambani, Bw Odinga alizidisha ushindani kati ya kiongozi wa chama cha Wiper na Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu ambao amewaahidi nyadhifa katika serikali yake iwapo Azimio itashinda.

Bw Odinga ameahidi Bw Musyoka wadhifa wa mkuu wa mawaziri huku akimshawishi Bi Ngilu kutotetea kiti chake akiahidi kumpa kazi katika serikali ya Azimio.

Wawili hao wamekuwa mahasimu wa kisiasa kwa muda, wakiwania ubabe wa siasa za eneo la Ukambani.

Katika kambi ya Dkt Ruto kuhusu eneo la Ukambani, uhasama umezidi kati ya aliyekuwa seneta wa Machakos , Bw Johnson Muthama na Gavana Alfred Mutua baada ya Naibu Rais kukumbatia Dkt Mutua wa Maendeleo Chap Chap.

Bw Muthama, ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto, ameapa kwamba hawezi kuketi katika jukwaa moja na Dkt Mutua ambaye inasemekana ameahidiwa wadhifa serikalini ikiwa Kenya Kwanza itashinda uchaguzi wa urais.

Hali ni sawa na hiyo katika eneo la Magharibi ambapo Dkt Ruto ameahidi kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi wadhifa wa mkuu wa mawaziri.

Kwa upande wake. Bw Odinga amemtengea Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya wadhifa wa waziri wa Fedha katika serikali ya Azimio, hatua ambayo wadadisi wanasema imezidisha joto la kisiasa katika eneo hilo.

“Dkt Ruto na Bw Odinga wamezidisha vita vya ubabe kwa kulenga kushawishi wapigakura kupitia mbinu ya kuahidi washirika wao nyadhifa katika serikali zao. Hii ndiyo hali inayoshuhudiwa Kakamega, Machakos, Kilifi na maeneo mengine,” akasema mchambuzi wa siasa Micheal Kwinga.

Katika Kaunti ya Kilifi, hatua ya Dkt Ruto kukumbatia Gavana Amason Kingi wa chama cha Pan African Alliance (PAA), haikumfurahisha mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ambaye anamezea mate kiti cha ugavana.

Bw Kingi alilenga kutwaa usemi wa siasa za eneo la Pwani ambako Bw Odinga ameahidi Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho wadhifa wa waziri wa Ardhi.

Bw Kwinga anasema hali hii imeshuhudiwa katika maeneo tofauti ambako Dkt Ruto na Bw Odinga wanalenga vigogo wa kisiasa kuvutia wapigakura.

“Kwa mfano ukiangalia eneo la Magharibi, Bw Mudavadi na Bw Oparanya walilengwa na mirengo yao na hii imepandisha joto la kisiasa. Wapigakura wamegawanyika, baadhi yao wakiunga Bw Odinga kwa kuahidi kumkabidhi naibu kiongozi wa ODM wizara ya Fedha na wengine wakiunga Dkt Ruto kwa kuahidi Mudavadi wadhifa sawa na wa waziri mkuu,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Angel Di Maria ajiunga na Juventus bila ada yoyote baada ya...

Ruto atanipigia magoti baada ya Agosti – Kiunjuri

T L