• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 11:59 AM
Sokomoko Ruto akiteua Naibu

Sokomoko Ruto akiteua Naibu

NA ONYANGO K’ONYANGO

JUHUDI za Naibu Rais William Ruto kutumia matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na chama chake kuamua ni nani anayefaa kuwa mgombea-mwenza wake ilitibuka pale washirika wake wawili kutoka Mlima Kenya walipotofautiana.

Kura hiyo iliyoendeshwa hivi majuzi ilimworodhesha Seneta wa Tharaka Nithi, Kithure Kindiki kuwa bora zaidi akifuatwa na Gavana wa Kirianyaga, Anne Waiguru.

Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua alikuwa wa tatu japo pengo kati ya watatu hao lilikuwa chini ya asilimia 5, kulingana na duru katika makazi rasmi ya Dkt Ruto katika mtaa wa Karen, Nairobi.

“Tulipaswa kuzingatia vigezo viwili ambavyo ni kura za maoni zilizoendeshwa na UDA katika eneo la Mlima Kenya na maeneo mengine ili kukadiria umaarufu wa viongozi hao. Matokeo yalipatikana na Kindiki akawa ndiye bora zaidi akifuatwa na Waiguri kisha Gachagua. Baadaye tulimwambia Naibu Rais aweke kando matokeo hayo kwa sababu pengo kati ya watatu hao lilikuwa finyu zaidi; lilikuwa asilimia mbili au tatu,” mbunge mmoja kutoka Mlima Kenya, ambaye aliomba tulibane jina lake alisema.

“Kufikia saa nane alasiri tulikuwa tumekubaliana kwamba Prof Kindiki ndiye aliyefaa. Kile kilichosalia kilikuwa ni kuwatuliza wawaniaji wengine, hasa Bw Gachagua, kwani tulikuwa na wawaniaji wengine kama vile Waiguru na Spika, Bw Justin Muturi,” mbunge huyo akaongeza.

Alisema kama wafuasi wa Dkt Ruto kutoka Mlima Kenya, walitaka mtu ambaye sifa zake zitakaribiana na za yule atakayeteuliwa na mgombea wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga.

Ingawa mapema wiki hii Naibu Rais alisema kazi ya kuteua mgombea mwenza wake ilikuwa rahisi, Jumamosi kibarua hicho kiligeuka kuwa kigumu.

Hii ni kwa sababu mbali na matokeo ya kura ya maoni, Dkt Ruto alilazimika kutoa nafasi kwa wabunge wandani wake kutoka Mlima Kenya kupiga kura ya siri hadi mwendo wa jioni.

“Suala la mgombea mwenza ni muhimu, lakini halitukoseshi usingizi. Hii ni kwa sababu muungano wetu unazingatia masuala yanayowahusu wananchi wala si nyadhifa za viongozi. Kwa hivyo, uteuzi wa mgombea mwenza ni rahisi zaidi,” akasema baada ya kumpokea rasmi kiongozi wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA), Gavana Amason Kingi.

Akaongeza: “Kama Kenya Kwanza, na kama mgombea urais katika uchaguzi mkuu ujao, tutahakikisha jina la mgombea mwenza wetu limewasilishwa kwa IEBC kabla ya muda wa makataa kukamilika.”

MLIMA KENYA

Lakini Jumamosi, suala hilo lilizua hali ya vuta nikuvute baada ya wabunge 30 kutoka Mlima Kenya waliokutana katika makazi ya Dkt Ruto, Karen, kusisitiza kuwa sharti wawe na usemi katika uamuzi huo.

Walisema hawangemruhusu Naibu Rais kufikia uamuzi huo kwa niaba yao.

“Kwa sababu nafasi hiyo ilikuwa imetengewa Mlima Kenya, ni sisi viongozi wa eneo hilo tunaopaswa kuamua ni nani anayefaa kuteuliwa. Awali, majina yalikuwa ni Kindiki na Gachagua na leo Jumapili orodha imepanuliwa kujumuisha Waiguru na Muturi. Tulimtaka Dkt Ruto atupe nafasi ya kuamua, hatutaki mtu mwingine atuamulie. Tulitaka kiongozi ambaye anaweza kuunganisha eneo la Mlima Kenya,” mbunge mwingine akasema.

Wakati wa upigaji wa kura ya moja kwa moja, Prof Kindiki alimshinda Bw Gachagua baada ya kupata kura 18 dhidi ya kura 10, zake mbunge huyo wa Mathira.

Hiyo iliwalazimisha viongozi hao kuoanisha matokeo hayo na matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na UDA yaliyowekwa wazi katika mkutano huo.

Wakati huo huo, maandamano yalitokea mjini Karatina, wafuasi wakipinga kile walichokitaja kama kuhujumiwa kwa Bw Gachagua.

Wakazi hao wapatao 1,000 waliokuwa wamepiga kambi katika mkahawa mmoja mjini humo, wakitarajia kupokea habari kuhusu uteuzi wa mbunge wao, waliondoka kwa hasira wakipinga hatua ya kuteuliwa kwa Kindiki kwa wadhifa huo.

Wengi wao waliimba “No Gachagua No Ruto” No Gachagua No Ruto” (Bila Gachagua hatutamkubali Ruto).

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo akaa ngumu, atishia kuwania urais

UDA: Ni tiketi ya Ruto-Gachagua

T L