• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Kalonzo akaa ngumu, atishia kuwania urais

Kalonzo akaa ngumu, atishia kuwania urais

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka anaendelea kukaa ngumu akishikilia kuwa ndiye anayefaa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga.

Imeibuka kuwa makamu rais huyo wa zamani anapanga kugombea urais iwapo hatateuliwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

Huku Bw Odinga akitarajia kutaja mshikilizi wa nafasi hii leo ama kesho, Bw Musyoka ameonya kwamba asipopewa nafasi hiyo huenda Bw Odinga asishinde urais Agosti 9.

Akiongea Ijumaa katika mkutano wa kisiasa katika kaunti ya Taita Taveta, makamu huyo wa rais wa zamani alifichua kuwa kuna watu wanaopanga kumnyima nafasi hiyo, akiwataja kama maadui wakubwa wa Azimio.

“Nimetembea safari ndefu ya kisiasa na Raila nilipomuunga mkono mara mbili kwa kuwa mgombeaji mwenza wake. Ikiwa ataamua kutoniteua kuwa naibu wake atafeli katika uchaguzi mkuu ujao,” Bw Musyoka akasema alipokuwa akiwapigia debe wawaniaji wa viti mbalimbali kwa tiketi ya Wiper katika kaunti ya Taita Taveta.

“Kuna njama inayoendeshwa na watu fulani kuninyima nafasi hiyo kutokana na sababu za kikabila. Kwa hivyo, ndugu yangu Raila asikubali kupotoshwa kwa sababu akifanya hivyo atakosa kushinda urais,” akaongeza.

Bw Musyoka alisema amefanya yote ambayo “nilipaswa kufanya ilhali kuna watu wanaofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa nimefeli kisiasa.”

Kiongozi huyo wa Wiper alisema hayo huku kukiwa na fununu kwamba huenda akawania urais kivyake ikiwa hatateuliwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

Mnamo Jumatatu, wandani wake walisema tayari wameanza kukusanya sahihi 2,000 kutoka angalau kaunti 24 nchini ili kumwezesha Bw Musyoka kuidhinishwa kuwania urais.

Sharti wagombeaji wa urais waandamanishe sahihi hizo pamoja na nakala za vitambulisho vya wafuasi wa mwaniaji urais ili aidhinishwe na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mbunge wa Wiper ambaye aliomba tulibane jina lake alisema walikamilisha shughuli ya kukusanya sahihi Ijumaa na Baraza Kuu la Usimamizi (MNC) liko tayari kupitisha hatua hiyo.

“Ikiwa Kalonzo hatateuliwa basi chama kiko tayari kumdhamini kama mgombea urais. Tulianza kukusanya sahihi Jumatatu na shughuli hiyo ikakamilika jana (mnamo Ijumaa),” akasema mwanasiasa huyo kutoka kaunti ya Makueni.

Mnamo Ijumaa, diwani Solomon Mghanga wa wadi ya Ngolia katika kaunti ya Taita Taveta, alithibitisha kuwa waliagizwa kukusanya sahihi ikiwa Bw Musyoka atakosa kuteuliwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

“Tuliamriwa kukusanya sahihi. Kila wadi ilipaswa kukusanya sahihi 150,” Bw Mghanga akanukuliwa akisema.

Mnamo Jumanne Bw Musyoka alijiwasilisha kuhojiwa na kamati maalum ya watu saba iliyobuniwa kusaka mtu anayehitimu kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Bw Odinga licha ya kuapa kutofika kwa mahojiano.Hii ni licha ya kwanza wiki jana, kiongozi huyu wa Wiper aliapa kutofika mbele ya kamati hiyo iliyoongozwa na Waziri wa zamani Noah Wekesa.

Akiongea na wanahabari Jumanne baada ya kuhojiwa Bw Musyoka akasema hivi: “Niliamua kufika mbele ya kamati hii ya watu mashuhuri ili kuzuia uwezekano wa watu fulani kutoa kizingizio kwamba nimewekwa kando kwa sababu nilikataa kuja.”

  • Tags

You can share this post!

Vijana wazima Sonko mkutano wa Azimio

Sokomoko Ruto akiteua Naibu

T L