• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Tim Wanyonyi tosha kwa ugavana wa Nairobi 2027- Raila

Tim Wanyonyi tosha kwa ugavana wa Nairobi 2027- Raila

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga amemwidhinisha Mbunge wa Westlands Timothy Wanyonyi kuwa mpeperushaji wa bendera ya ODM katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi ifikapo mwaka 2027.

Akiongea Jumatano, Novemba 15, 2023, alipokutana na viongozi wa kidini katika Shule ya Msingi ya Westlands, Bw Odinga alisema Azimio ilipoteza ugavana wa Nairobi 2022 kutokana na kile alichokitaja kama “udhaifu” wa mgombeaji wake Polycarp Igathe.

Bw Wanyonyi alikuwa ameonyesha nia ya kuwania ugavana wa Nairobi kwa tiketi ya ODM lakini akashauriwa kumpisha Bw Igathe wa chama cha Jubilee. Vyama hivyo viwili ni washirika wakuu katika muungano wa Azimio.

“Naomba msamaha kwa kushauriwa kuwa tuunge mkono mtu mwingine katika uchaguzi wa ugavana badala ya Tim. Bw Tim alikuwa mkarimu na akakubali. Tulitaka awe mgombeaji mwenza wa Igathe lakini akakataa. Badala yake aliamua kurudi kuwa Mbunge wa Westlands,” Bw Odinga akasema.

Duru zilisema kuwa Bw Igathe alipendekezwa kuwania kiti hicho na Rais wa nne Uhuru Kenyatta ambaye ni kiongozi wa Jubilee na mwenyekiti wa Baraza Kuu la Muungano wa Azimio.

Hiyo ndiyo maana ODM ilimshauri Bw Wanyonyi kujiondoa kinyang’anyironi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wafuasi wote wa Azimio wanaelekeza kura za ugavana katika kapu moja.

Hata hivyo, Bw Igathe alibwagwa na mgombeaji wa Kenya Kwanza Johnson Sakaja licha ya Azimio kushinda idadi kubwa ya madiwani.

Bw Sakaja alizoa jumla ya kura 699,392 huku Bw Igathe akipata kura 573,518 kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Afisa wa Uchaguzi katika kaunti ya Nairobi Albert Gogo.

  • Tags

You can share this post!

Mafuta ya Sh17b yalikuwa ya serikali, sio ya mfanyabiashara...

Mbunge atuza watoto zawadi ya ‘kipekee’

T L