• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mbunge atuza watoto zawadi ya ‘kipekee’

Mbunge atuza watoto zawadi ya ‘kipekee’

NA LUCY MKANYIKA

KATIKA utamaduni wa Kiafrika, mtoto anapozaliwa, wanakijiji hutembelea wazazi ili kutoa zawadi.

Hata hivyo, Mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako anaendeleza mbinu ya kipekee na mpango wake wa “Mtimtoto” unaohusisha kutoa miche kwa kila mtoto anayezaliwa katika eneo hilo.

Badala ya kuwazawidi wazazi kwa pesa, nepi au nguo za mtoto, mbunge huyo huwapa wazazi miche 10 ambapo mitano hupandwa nyumbani na iliyobaki ikipandwa katika shule ambayo mtoto huyo anatarajiwa kusoma.

“Lengo letu ni kuhakikisha upanzi wa miti unakuwa kitu cha kawaida. Hatutaki ufanyike kama tukio la mara moja. Tunataka kila mtu ajue umuhimu wa kuokoa na kutunza mazingira yetu,” alisema Bw Mwashako.

Mpango huu unalenga kukuza uhifadhi wa mazingira na kufanya wakazi kuwajibika tangu utotoni.

Kwa mujibu wa Bw Mwashako, kufikia sasa, watoto 6,400 wamefaidika na mpango huu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita huku asilimia 95 ya miche hiyo ikiendelea kunawiri.

“Mradi huu unasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake mbaya,” alisema.

Mkazi mmoja, Bi Phoebe Wakio, aliyepokea miche hiyo alipomzaa mwanawe mwaka wa 2019, anasema wanaendelea kutunza miti hiyo.

Vilevile, alisema anawafundisha watoto wake umuhimu wa kuhifadhi mazingira na jukumu wanaloweza kutekeleza katika uhifadhi wa miti kwa vizazi vijavyo.

“Tumekuwa tukiitunza tangu wakati huo na miti imekua sana. Mradi huu sio tu kuhusu kupanda miti kwa ajili ya watoto wetu, lakini pia kuhusu kuwafunza watoto wetu uwajibikaji kwa mazingira yao,” alisema.

Huku nchi ikipania kupanda takriban miti bilioni 15, Kaunti ya Taita Taveta inalenga kupanda miti milioni 4.3 mwaka huu.

Kamishna wa kaunti hiyo, Bi Josephine Onunga ametangaza mpango wa kuongeza misitu katika eneo hilo kwa kuhusisha watoto wa shule katika mpango wa upanzi wa miti.

Kuanzia Januari, shule zitakapofunguliwa, kila mwanafunzi atapangiwa mti ambapo ataupanda na kuutunza.

“Hata wale ambao wanaendelea kufanya mtihani wao wa KCSE watapanda mti ili kuadhimisha siku ambayo walikamilisha mtihani wao,” alisema.

Mnamo Jumatatu pekee, zaidi ya miti 73,000 ilipandwa katika kaunti hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Tim Wanyonyi tosha kwa ugavana wa Nairobi 2027- Raila

Mpenzi aliniacha kwa kumtamani rafikiye; nishauri sababu...

T L